OR-TAMISEMI
Wazee Wilayani Rufiji wamefanya Dua ya kumuombea Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Rufiji Mhe. Mohamed Mchengerwa ya kumtakia heri katika utekelezaji wa majukumu yake ya kitaifa pamoja na jukumu la kuijenga Rufiji kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo
Dua hiyo imefanyika katika Msikiti Mkuu wa Jumuiya ya Ikwiriri na Mitaa mbalimbali ya Ikwiriri, ambapo wananchi wa Rufiji wamepata fursa ya kuwaombea waliotangulia mbele za haki, kuliombea Taifa liendelee kuwa na amani na utulivu, pamoja na kumuombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na viongozi aliwateua ili waendelee kulitumia taifa kwa uzalendo.
Wakizungumza katika Mahojiano Maalumu Wazee hao, akiwemo Daruesh Rwanda Mkazi wa Ikwiriri amesema Dua imelenga kumuombea Mhe. Mchengerwa kwasababu ameleta maendeleo, amani na utulivu ndani ya Rufiji.
“Ametuletea maendeleo na ametutengenezea amani, sasa hivi wafugaji wapo sehemu yao na sisi tupo sehemu yetu hivyo maisha mazuri yanaendelea” amesema Rwanda.
Kiongozi wa Al Qadiri ya Wilaya ya Rufiji, Yusufu Kinjogo amempongeza Waziri Mchengerwa kwa namna alivyoiletea Rufiji maendeleo ambayo yameleta mabadiliko ya kifikra kwa wananchi.
“Tunamshukuru kwa kuibadilisha Rufiji, Rufiji ya leo imebadilika kwani mitaa yote imewekwa lami, Mungu ampe afya njema ili aendelee kuwatumikia wananchi,” amesema Kinjojo.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa amewashukuru wote waliandaa Dua hiyo ya kumuombea, kuwaombea Viongozi waliotangulia mbele za haki, kuliombea Taifa pamoja na viongozi wa Serikali ambao wanaongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
“Nawashukuru sana wazee wa Rufiji, leo tumewakumbuka wazee wetu waliotangulia mbele za haki, tumemkumbuka Mtume wetu Mohamed (S.A.W), tumemuombea Mhe. Rais na viongozi aliowateua katika nafasi mbalimbali na tumeiombea Rufiji ili iendelee kupata maendeleo,” Amesema Mhe. Mchengerwa.
The post WAZEE RUFIJI WAMUOMBEA DUA WAZIRI MCHENGERWA KUTOKANA UTENDAJI KAZI WAKE MZURI appeared first on Mzalendo.