
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeamua kubadili utaratibu wa kuponya majeraha ya viongozi na wanachama wa chama hicho yaliyotokana na uchaguzi mkuu wake uliomalizika Januari 22, 2025.
Kabla na baada ya uchaguzi huo, kumeshuhudiwa minyukano mikali kutoka kwa makundi mawili ya Tundu Lissu na Freeman Mbowe, ambao kwenye uchaguzi walikuwa wakiwania nafasi ya uenyekiti.
Nguli hao wa siasa za upinzani waliwagawa wanachama na viongozi wake kwa kila kundi kumnadi mgombea wake. Kila mbinu zilitumika, ikiwamo za kutoleana shutuma hata za rushwa.
Mwisho wa uchaguzi, Lissu ambaye alikuwa Makamu mwenyekiti bara, akachaguliwa kuwa mwenyekiti kwa kura 513 sawa na asilimia 51.5, huku Mbowe aliyekuwa akitetea nafasi hiyo aliyoiongoza kwa miaka 21, akipata kura 482, sawa na asilimia 48.3 huku Odero Charles akipata kura moja. Idadi ya kura ilikuwa 999, huku kura tatu zikiharibika.
Mbali na Lissu, John Heche alichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti Bara na alikuwa akimuunga mkono Lissu, akimbwaga Ezekiel Wenje ambaye alikuwa akimuunga mkono Mbowe.
Mbowe ambaye kwa mujibu wa Katiba ya Chadema anakuwa mjumbe wa kudumu wa Kamati Kuu, alikubali matokeo na moja ya salamu zake kwa wajumbe wa mkutano mkuu katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam akiwaaga alisema: “Tumemaliza uchaguzi huu, lakini uchaguzi huu umeacha majeraha mengi kwa chama chetu, ushauri wangu kwa viongozi wetu, kakiponyeni chama chetu.”
“Mimi niliahidi ningeshinda ningeunda tume ya ukweli na maridhiano, watu wakazungumze yaliyojiri kwenye uchaguzi huu, watu walipokoseana, walipokosana, walipokosa maadili, walipokibagaza chama chetu, wakasameheane wapeane mikono ili chama chetu kiwe na nguvu zaidi,” alisema Mbowe.
Mbowe, aliyekaa madarakani kwa miaka 21 akipokea kijiti kutoka kwa Bob Makani alisema: “Kama mnaniheshimu kama mtu niliyekifanyia kazi chama hiki, nawaagiza haraka kaundeni tume ya ukweli na upatanishi, mkatibu majeraha ili muweze kujenga umoja. Ushindi wowote ni ushindi wa chama, asitokee mmoja wetu akaleta kiburi cha uchaguzi. Oneni ulazima wa kutibu majeraha ya mchakato wa uchaguzi.”
Baada ya uongozi mpya chini ya Mwenyekiti wa Lissu na viongozi wengine wapya kuanza kazi, walienda kujifungia Bagamoyo, mkoani Pwani, pamoja na mambo mengine, walijadiliana namna ya kuja na njia bora ya kutibu majeraha hayo.
Kwa nini wazee?
Jumapili ya Januari 23, 2025, Mwananchi lilifanya mahojiano maalumu na Lissu nyumbani kwake, Tegeta jijini Dar es Salaam, ambaye alijibu kwa kina swali aliloulizwa juu ya ombi la mtangulizi wake (Mbowe) la kuundwa kwa kamati kutibu majeraha limefikia wapi.
Lissu alisema walizungumza kwenye kamati kuu iliyoketi Bagamoyo na kukubaliana jukumu hilo lifanywe na Baraza la Wazee.
“Tumezungumza katika Kamati Kuu iliyokaa Bagamoyo njia bora zaidi ya kuponyana majeraha ya uchaguzi, sio kuunda tume ya upatanishi na ukweli kama alivyopendekeza Mwenyekiti (Mbowe), pengine njia bora zaidi siyo kuunda kamati, badala yake, tuangalie utaratibu uliopo wa chama chetu, kwani kina baraza la wazee wa chama,” alisema.
“Tutumie chombo cha wazee wa chama kusaidia kuponya masuala yaliyotokana na uchaguzi pamoja na majeraha yake, kuunda kamati ya upatanishi ya aina hiyo na lugha inayotumika ni kamati ya ukweli na patanishi kwa muundo wa kamati hizo ni kamati za kiserikali,” alisema.
Katika kuifafanua hoja yake hiyo, Lissu, ambaye kitaaluma ni mwanasheria alitolea mfano Tume ya Desmond Tutu, aliyekuwa Askofu wa Kanisa Anglikana nchini Afrika Kusini au ile ya upatanishi ya Kenya na ya Uganda. Alisema kuna mfumo kama huo kwa nchi mbalimbali.
“Tukienda na mfumo kama wa tume zilizopo, hizi tume zitakuwa zinafanya vikao kwa kufanya mikutano ya hadhara na watakuja kuzungumza hadharani mambo wanayojua na waliyotendewa na waliyoyatenda sasa, kufanya hivyo ni kuwa tayari na matokeo,” alisema.
Alipoulizwa jukumu hilo la Baraza la Wazee wa Chadema (Bazecha), kutibu majeraha hayo litaisha lini? Lissu alisema kwa kuwa tatizo hilo ni kubwa kuanzia ngazi ya matawi, litachukua muda mrefu.
“Jukumu la kuponyesha majeraha litachukua muda mrefu, tatizo hili ni kubwa, lilianzia tangu kwenye chaguzi za chini kabisa, kwa hiyo si la kuisha sasa na ndiyo maana nikiona inaendelea hainishangazi, lakini matumaini yangu wazee watamaliza kazi hiyo,” alisema.
Lissu alisema katika kikao walichofanya Bagamoyo walijiuliza chama cha siasa cha upinzani katika mazingira halisi ya Tanzania ambayo wote wanaotaka kujua wanajua na kuwindwa usiku na mchana kutekwa au kuuawa na kuchafuliwa itakuwaje? Jibu walilopata si vizuri kuundwa kwa tume.
“Tukienda na kamati ya ukweli na upatanishi ya aina hii tutafika wapi? Busara zetu zikatuambia badala ya kwenda na njia hiyo, tutumie njia ya wazee wa chama, na utaratibu utakao tumika ni huo wa wazee wa chama, kwa sababu wapo,” alisema. Kulingana na maelezo ya Lissu, anawaamini wazee watatimiza jukumu hilo kwa kuwa wakati wa uchaguzi walifanya kazi kubwa ya kuzungumza na kutuliza makali ya kampeni, huku akieleza wazee wa chama hicho ni chombo rasmi na ni muhimu kitumike.
“Katika kila ngazi ya chama wazee wapo, kwa hiyo hakuhitajiki kuwa na kamati ya watu watano, 10 au 20 ikafanya hiyo kazi, manake ukitaka ifanye kazi kisawasawa inabidi iende kila mkoa kwa sababu uchaguzi umefanyika nchi nzima,” alisema.
Lissu alisema chombo hicho tayari kimeanza kazi, ingawa bado hajaonana nacho tangu akipatie majukumu hayo, huku akieleza atakuwa anakutana nacho mara kwa mara kufanya vikao na hawapaswi kusubiri hadi Mwenyekiti apulize kipyenga kwa kuwa kilishapulizwa.
Alisema kwa kuwa Chadema kina mfumo kutoka ngazi ya juu hadi chini, anaamini kamati kuu ikishatoa maelekezo kama ilivyofanya wakati wa uchaguzi huo, yanatakiwa kwenda sehemu zote na kutekelezwa.
Mabadiliko ya Katiba ya Chadema
Mbali na kulipatia jukumu Baraza la Wazee, Lissu alisema katika kikao kilichofanyika Bagamoyo walikubaliana kufanya mabadiliko ya katiba ya chama hicho kwa kuyatazama maeneo yanayosababisha changamoto za uchaguzi ziendelee.
“Kuponya majeraha ni mchakato endelevu na si haya tu, tukiwa Bagamoyo tumezungumzia mambo haya yametokana na mfumo wetu wa kikatiba ndiyo unasababisha matatizo ya aina hii, haitatosha kuelezana nani alimkosea mwenzake na wapi, inatakiwa kuangalia utaratibu wetu wa kikatiba,” alisema.
Alisema ni lazima Katiba itazamwe na namna ya kurekebishwa, mathalani utaratibu wa kikatiba uliopo kwa sasa wa chama hicho, unatengeneza matatizo yanayofanya yaendelee.
“Mfano watu wanaosimamia uchaguzi ngazi ya kata, viongozi ni viongozi kutoka ngazi ya jimbo au wilaya, wakiharibu au kuwa na malalamiko yanaenda kusikilizwa ngazi ya juu ya jimbo na waliosimamia ni kina nani? Mana yake wanakuja kusimamia rufaa ya uchaguzi waliosimamia wenyewe,” alisema.
Lissu alihoji kama walikosea wao watajitangaza?
“Sisi hapa tuliboronga, ni kitu ambacho hakiwezekani na hivyo hivyo uchaguzi ngazi ya kanda unasimamiwa na ngazi ya Taifa ambayo ni Kamati Kuu, ukiboronga hapo unaenda wapi na kikatiba ngazi ya juu ni Kamati Kuu,” alisema.
Lissu alisema kwa mfumo huo tu, Katiba ya chama hicho imetengeneza mazingira ambayo haki haitatimia na kusema kumekuwa na malalamiko nchi nzima kwamba utaratibu wa rufaa hautekelezeki.
Utaratibu upi sahihi?
Lissu anasema kama wanazungumzia Tume huru ya uchaguzi, na suala hilo linatakiwa kuanza na Chadema wenyewe. Kwanza kwa namna ya kuendesha chaguzi za haki na kutengeneza chombo ndani ya chama ambacho kitasimamia chaguzi zao za ndani.
“Tunatakiwa kuwa na chombo kingine ambacho kitashughulikia malalamiko ya uchaguzi, kwa hiyo kunakuwa na Tume ya Uchaguzi ndani ya chama ambayo wajumbe wake hawahusiani na hii michakato ya kugombania au maslahi katika vinyang’anyiro vinavyoendelea itakuwa vizuri,” alisema.
Alisema kazi yao itakuwa kusimamia kwa kuangalia anayestahili kugombea anapataje fomu na yote hayo yatafanywa na bodi ya uchaguzi, lakini pia kuwe na bodi nyingine itakayoshughulikia malalamiko ya uchaguzi.
“Bodi ya malalamiko vilevile itakuwa na watu wa chama lakini hawajihusishi na shughuli za kila siku za uongozi wa chama au usimamizi wa uchaguzi, tukifanya hivi malalamiko ya sasa kwamba viongozi wanapanga safu kwa kuhakikisha watu wao wanawekwa na wapinzani wao kuenguliwa na rufaa hazifanyiwi kazi, kelele hizo ama zitaisha kabisa kwa sababu wanaogombea wanakuwa hawana mamlaka yoyote,” alisema.
Bazecha mguu sawa
Mwenyekiti wa Bazecha, Suzan Lyimo amekiri kupewa jukumu hilo na tayari ameshaunda timu ya watu tisa ya wazee wastaafu wa kuanzia miaka 59 na kuendelea, ambao hawana nafasi yoyote ndani ya chama hicho waweze kusimamia jukumu hilo.
“Tumeshaunda timu ya wazee tisa wastaafu ambao hawana nafasi yoyote ya chama kuanzia miaka 59 na kuendelea, tutaanza kikao cha kwanza tuweze kukutana hivi karibuni kujadiliana kwa kuwa bado mambo hayajakaa sawa,” alisema.
Lyimo alisema ameshawapa taarifa wazee wa chama hicho nchi nzima, huku akieleza mpango wao unalenga kuanzia ngazi ya majimbo, na tayari Mkoa wa Kilimanjaro wameshaanza kazi ya kuzungumzia jambo hilo.
Katika maelezo yake, Lyimo alisema kilichobakia ni kumpelekea taarifa Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika ili waweze kukutana pamoja na kupeana hadidu za rejea.
‘Njia sahihi iliyotumika’
Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Conrad Masabo ameunga mkono uamuzi wa kutumia muktadha wa Baraza la Wazee kutibu majeraha hayo.
“Lissu anaondoka kama moja ya waathirika wa huo mgogoro na kuwaachia watu wengine wawasaidie kwa sababu huwezi kuamua kesi yako, Lissu akisimamia yeye mwenyewe alikuwa mtuhumiwa muumizaji na muumizwa atafanyaje hiyo kazi,” alisema.
Dk Masabo katika maelezo yake alisema jambo hilo la kuumizwa likitazamwa kwa muktadha wa Kiafrika, wazee wanaweza kusimama katikati kwa kuwa lilisimamia uchaguzi ambao ulikubalika, nadhani wanaweza kulifanya jukumu hilo.
“Kiafrika siku zote wazee ni wasuluhishi na mtu akisema hataki basi huyo anakuwa ana shari kwa sababu wazee wana uwezo wa kumkemea Lissu na mtu mwingine yeyote kwa hulka ya Kiafrika,” alisema.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini ya Chadema, Profesa Azaveli Lwaitama alisema uamuzi wa kamati kuu kulipatia Baraza jukumu hilo lifanye kazi hiyo ni sahihi, huku akisema itasaidia kuepuka minong’ono ya pembeni kwamba wametengeneza vitu ambavyo havipo kisheria.
“Siasa za rika hili ni siasa za moto moto, lazima utengeneze wazee, wanaweza kukuheshimu na wakapishana na wewe kwa hoja lakini akaendelea kukuheshimu na hawezi kutoka pale kwenda kusema sema mahali popote kwa sababu lengo ni kujenga,” alisema.
Profesa Lwaitama katika maelezo yake alisema ana imani jambo alilolisema litakuwa limejenga vile inavyotakiwa kwenye misingi ya kikatiba ya chama hicho, Baraza la wazee litafute utaratibu wa kufuata hoja ya ‘stronger together.’
Walijiandaa kwa uchaguzi?
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Matrona Kabyemela anasema baraza la wazee na kutibu majeraha itategemea namna upande unaohisi majeraha utakavyopokea hiyo taasisi.
“Je, baraza lina uwakilishi mzuri wa pande zote mbili? Je, liko katikati na je, lina maono ya kurudisha umoja na mshikamano ili taasisi iendelee vizuri? Haya ndiyo ya kuzingatiwa na mwenyekiti mpya ili kujenga chama chenye umoja wa kidemokrasia,” alisema.
Matrona alisema ni muhimu wagombea na wafuasi wao wawe wanajiuliza maswali hapo kabla ya kuingia kwenye kinyang’anyiro chochote kuna kushinda na kukosa ili kupunguza majeraha ambayo yanaweza kugharimu taasisi yoyote.
“Hawa wote kabla ya kuingia kwenye uchaguzi walitakiwa wajiulize maswali manne ya mlinganyo wa kushinda na kushindwa kabla ya kuingia kwenye kinyang’anyiro, unashinda nini unaposhinda?
“Unapoteza nini unaposhinda? unashindwa nini unaposhindwa na unashinda nini unaposhindwa. Haya maswali husaidia wagombea na wafuasi wao kujiandaa na kutokupata majeraha, maana kushindwa hakumaanishi kapoteza kabisa, kuna vitu amevishinda,” alisema.