Wazazi wakumbushwa kuwalinda watoto wao na msongo wa mawazo

Arusha. Wazazi na walezi nchini wametakiwa kuchukua tahadhari dhidi ya hali ya msongo wa mawazo unaowakumba watoto wao ili kuwaepusha na magonjwa yasiyoambukiza na pia hatua za kujidhuru.

Hayo yamejiri wakati matukio ya watoto kujinyonga yakizidi kushamiri nchini yakiwemo ya watatu wa Mkoa wa Arusha waliojinyonga kwa nyakati tofauti mwaka jana akiwemo Lukuman Hussein (9), Yusuph Laizer (13) na Witness Pastory.

Kutokana na hayo, wazazi na walezi wametakiwa kukabiliana na hali hiyo kwa kuongeza ukaribu na kuzungumza na watoto wao mara kwa mara ili kujua mwenendo wa maisha yao ya kila siku.

Ushauri huo umetolewa leo Februari 22, 2025 kwenye kikao kazi cha Mkoa wa Arusha cha kupitia utekelezaji wa programu jumuishi ya malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto inayotekelezwa na serikali kupitia idara za elimu ya msingi, afya, ustawi wa jamii na lishe kwa kushirikiana na wadau binafsi.

Akizungumza kwenye kikao hicho, Zukra Kalunde kutoka shirika la kupinga matukio ya ukatili ‘Fikiso’ amesema kuwa kumekuwa na wimbi kubwa la watoto wanaokabiliwa na msongo wa mawazo kutokana na matukio ya ukatili wanayokumbana nayo katika jamii inayowazunguka.

“Matukio hayo ambayo mbaya zaidi yanatekelezwa na watu wao wa karibu, wakiwemo walezi, ndugu au hata walimu wao, yamekuwa yakiwaingiza watoto kwenye msongo mkubwa wa mawazo huku wakikosa mtu wa karibu wa kumshirikisha na mwisho kuamua kuchukua uamuzi mbaya ikiwemo kukimbia makazi yao au hata kujidhuru,” amesema.

Ofisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Monduli, Hendry Laizer amesema kwa sasa wanaunda mabaraza na mabalozi kwenye jamii zao za Kimasai ili kukabiliana na matukio ya ukatili kwa watoto.

“Tunajenga uwezo kwenye ngazi ya jamii kukabiliana na matukio hayo baada ya kubaini familia nyingi za jamii ya kifugaji wanashikilia mila na desturi ambazo nyingine sio rafiki kwa watoto,” amesema.

Naye, Ofisa Ustawi wa Jamii jiji la Arusha, Nivo Kikavu amesema kuwa changamoto ya malezi na makuzi katika eneo lake ni watoto wanaotembea na wazazi wao wanaofanya biashara katika masoko ya Kilombero, Samunge na Soko Kuu.

“Kwa sasa tumejenga vituo vya malezi katika maeneo ya karibu ambayo tunawahamasisha wapeleke watoto wao kwenye vituo kuliko kutembea nao migongoni na wakati mwingine kuwaachia wanazurura ndani ya masoko na kushuhudia matukio mengi ambayo hayana afya katika maisha yao,” amesema.

Akifungua kikao hicho, Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Arusha, Sarah Mlaki amesema suala la malezi ya watoto imekuwa changamoto na kuwataka maofisa ustawi wa jamii na maendeleo ya jamii kushirikiana na wadau binafsi kuhakikisha usalama wa watoto nchini unatekelezwa.

“Lakini pia kutokana na ukosefu wa uwiano sawa wa huduma za malezi, makuzi na lishe kwa vijijini na mijini hasa kutokana na mashirika mengi kuwa mijini, nawaagiza kila halmashauri katika idara zilizoko kwenye mpango huu, mtenge bajeti ya utekelezaji ili kusaidia na watoto wa vijijini wapate huduma sawa na wale wa mijini,” amesema.

Zaidi amewataka kubadilishana taarifa za matukio yanayotokea na jinsi wanavyokabiliana nazo ili kusaidia wengine katika maeneo mengine kuchukua tahadhari.