Wazayuni wamekithiri kumwaga damu za watoto Ghaza, kila nusu saa mtoto mmoja anakufa shahidi

Kituo cha Habari cha Palestina kimetangaza kuwa, watoto 17,400 wa Kipalestina wameuawa shahidi tangu yalipoanza mashambulizi ya kinyama ya utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Ghaza tarehe 7 Oktoba mwaka jana.

Kituo hicho cha habari kimeeleza katika ripoti yake kuwa: kuuliwa shahidi watoto hao 17,400 Wapalestina na utawala wa Kizayuni kunaonyesha kuwa katika kila dakika 30 mtoto mmoja huuawa shahidi katika Ukanda wa Ghaza.

Ripoti hiyo imeongezea kwa kusema: watoto 710 Wapalestina kati ya hao waliouawa shahidi walikuwa na umri wa chini ya mwaka mmoja, yaani walizaliwa vitani na waliuawa shahidi katika vita.

Ripoti ya Kituo cha Habari cha Palestina, imeendelea kueleza kuwa, watoto 1,793 kati ya waliouawa shahidi walikuwa na umri wa mwaka mmoja hadi mitatu, 1,205 walikuwa na umri wa miaka minne hadi mitano, 4,205 walikuwa na umri wa miaka sita hadi 12, na 3,442 miaka 13 hadi 17.

Ikumbukwe kuwa, kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Afya ya Palestina, tangu yalipoanza mashambulizi ya kinyama na mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala wa Kizayuni huko Ghaza tarehe 7 Oktoba mwaka jana, Wapalestina 44,235 wameuawa shahidi na 104,638 wamejeruhiwa wengi wao wakiwa wanawake na watoto…/