
Bukavu. Wakati kundi la Wazalendo likijipa jukumu la kuwazuia waasi wa M23 kuutwaa mji wa Uvira, baadhi ya askari wa Jeshi la Jeshi la Ulinzi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), FARDC wameripotiwa kuingia mitini.
Jeshi la FARDC limewataka askari wake waliotoroka kurejea kwenye vikosi vyao, huku wapiganaji wa kundi la M23 wakidaiwa kuuteka Mji wa Lubero, uliopo Jimbo la Kivu Kaskazini Mashariki mwa DRC.
Shirika la Habari la Uingereza (Reuters) limeripoti leo Ijumaa Februari 21, 2025, kuwa baadhi ya askari wa FARDC waliokuwa katika mapigano makali na wapiganaji wa M23, walianza kukimbia, huku wengine wakitoroka kambini kwa hofu ya kukutana na waasi hao.
Ghasia hizo zinaashiria hali ya kuvurugika kwa jeshi la FARDC mbele ya mashambulizi ya M23, kundi la waasi ambalo limeiteka miji miwili mikubwa mashariki mwa DRC – ya Goma na Bukavu na kuzua hofu vikubwa zaidi.
Taarifa ya Msemaji wa Jeshi la FARDC katika Jimbo la Kivu Kaskazini, imewataka wanajeshi waliotoroka Lubero warudi kwenye nafasi zao ndani ya saa 12 na askari wote waepuke uporaji wa mali za raia na vitendo vingine vya uhalifu.
Mapigano ya FARDC na M23 yameendelea kusini mwa Lubero, Mji uliopo Kivu Kaskazini kwa saa 72 zilizopita, Msemaji wa FARDC, Sylvain Ekenge amesema.
Wazalendo wailinda Uvira
Upande wa Kivu Kaskazini, M23 wanaendelea kupambana kuyatwaa maeneo yote ya jimbo hilo ikiwemo Lubero huku Jimbo la Kivu Kusini wapiganaji wa kikosi cha Wazalendo, wakipambana kuzuia M23 wasiutwae Mji wa Uvira.
Wapiganaji wa kikosi cha Wazalendo wamelazimika kusimama kidete kutetea Mji wa Uvira dhidi ya wapiganaji wa M23, baada ya askari wa FARDC kudaiwa kutoroka mapigano, huku wengine wakidandia mitumbwi na kutorokea Kalemie nchini humo.
Asubuhi ya Alhamisi, wakazi watano wa mji wa Lubero walielezea hali ya mapigano na wanajeshi waliotoroka kutoka mstari wa mbele pamoja na vitendo vya uporaji katika soko kuu na maduka ya simu na nguo.
“Hali ni ya vurugu kabisa Lubero. Risasi zinapigwa, wanajeshi wanakimbia ovyo,” amesema mmoja wa wakazi hao, akizungumza kwa masharti ya kutotajwa jina kwa sababu za kiusalama.
Baadaye, msimamizi wa kijeshi wa Lubero, Alain Kiwewa, amesema utulivu umerejeshwa katika mji huo lakini akawalaumu wanajeshi wasio na nidhamu kwa kutoroka mapigano na kuibua hofu kwa jamii.
Matukio haya na kuzuka upya kwa mapigano na M23 karibu na Lubero yameongeza shinikizo kwa FARDC.
Jeshi hilo lilirejea kwa kujihami katika jimbo jirani la Kivu Kusini baada ya wapiganaji wa M23 kuutwaa mji mkuu wa jimbo hilo, Bukavu mwishoni mwa wiki, hali iliyosababisha mapigano kati ya vikosi vya FARDC na wanamgambo washirika waliotaka kubaki na kupigana.
Kuongezeka kwa mapigano kumewatia wasiwasi viongozi wa kanda na jumuiya ya kimataifa.
Vikwazo kwa Waziri wa Rwanda
Jana Alhamisi Februari 20, Marekani iliweka vikwazo dhidi ya waziri mmoja wa Serikali ya Rwanda ambaye anadaiwa kuwa na mkono wake miongoni mwa watu wanaofadhili wapiganaji wa M23 wanaoitesa Serikali ya DRC.
Hata hivyo, Rwanda ambayo inapakana na DRC, inakanusha madai ya Congo na Umoja wa Mataifa (UN) kwamba inawafadhili M23 kwa silaha na wanajeshi, badala yake imekuwa ikidai kuwa uwepo wa askari wa Jeshi la Ulinzi la Rwanda unalenga kuilinda mipaka dhidi ya wapiganaji wa Kihutu waliotorokea DRC.
Hata Rais Paul Kagame wa Rwanda, alipofanya mahojiano ya CNN, alidai kutokuwa na taarifa ya uwepo wa askari wa jeshi lake ndani ya mipaka ya DRC, huku akidai wapiganaji wa Kihutu anaowawinda wanapigana bega kwa bega na FARDC.
DRC inakataa madai hayo ikisema Rwanda imekuwa ikitumia M23 kama wakala wa kupora madini yake, kama dhahabu na koltani, madini yanayotumika kutengeneza simu janja na kompyuta.
Jana Alhamisi, Wizara ya Fedha ya DRC imetangaza kuanzishwa kwa mfuko wa mshikamano wa kusaidia jeshi, ambapo wananchi, kampuni na mashirika wanaweza kuchangia moja kwa moja mapigano mashariki mwa nchi hiyo.
Hatua hiyo inaonyesha uwepo wa mzigo wa kifedha wa uasi, ambao umeliwezesha kundi la M23 kuteka maeneo makubwa ya ardhi ya Congo na maeneo muhimu ya uchimbaji madini.
Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa Mashirika