Wayemen wawapa indhari Waarabu wenzao: Nia ya Israel ni ‘kuyatumikisha mataifa yote ya Kiarabu’

Mamilioni ya waandamanaji waliokusanyika katika mji mkuu wa Yemen, Sana’a na katika miji mingine mingi ya nchi hiyo wametangaza uungaji mkono wao kwa Muqawama wa Palestina na Lebanon, wakionya dhidi ya njama za Israel za kuzitumikisha na kuzifanya watumwa wake nchi zote za Kiarabu.

Katika mikusanyiko hiyo mikubwa iliyopewa jina la “Uaminifu kwa Viongozi wa Mashahidi… Pamoja na Ghaza na Lebanon Hadi Ushindi”, wananchi wa Yemen walibeba bendera za nchi hiyo, za Palestina na Lebanon sambamba na picha za viongozi wa harakati za Muqawama za Lebanon na Palestina, Hizbullah na Hamas, ambao wameuliwa shahidi na utawala ghasibu wa Israel.

Aidha, wamelaani mauaji ya kikatili ya halaiki yanayoendelea kufanywa na utawala dhalimu wa Kizayuni, kuwahamisha Wapalestina kwa nguvu katika makazi yao na mauaji ya kimbari dhidi ya wananchi hao madhulumu unayoyafanya kwa msaada wa Magharibi.

Katika maandamano na mikusanyiko hiyo iliyofanyika jana baada ya Sala ya Ijumaa, wananchi wa Yemen wamelaani pia ushiriki wa Jamii ya Kimataifa na kimya na kutochukua hatua nchi za Kiarabu na Kiislamu za kukabiliana na uvamizi na jinai za Israel dhidi ya watu wa Ghaza na Lebanon.

Wananchi hao wamesisitizia pia dhamira yao ya kuunga mkono Ghaza Palestina na Lebanon na utayari wao wa kukabiliana na hatua zozote za kichokozi za Marekani, Israel na Uingereza.

Katika taarifa waliyotoa baada ya mikusanyiko hiyo, waandamanaji hao walisema, uvamizi wa Israel umevuka mipaka ya Ghaza na kufika Lebanon na Ukingo wa Magharibi huku jamii ya kimataifa ikiendelea kuonyesha kimya kizito.

Wananchi wa Yemen wameahidi kuendelea kufanya maandamano kila wiki kuonyesha mshikamano na wananchi wa Palestina na Lebanon hadi ushindi utakapopatikana.

Vilevile wametoa salamu zao za rambirambi kwa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Hizbullah na nchi za Kiarabu na Kiislamu kufuatia kuuawa shahidi Mkuu wa Baraza la Utendaji la harakati hiyo Sayyed Hashem Safiyyuddin, na kuapa kuwa wataendelea kuuenzi urithi wake na urithi ulioachwa na viongozi wengine wa Muqawama waliouawa shahidi…/