Wawili wanaswa na noti bandia Mbeya, madereva saba wafungiwa leseni

Mbeya. Jeshi la Polisi mkoani Mbeya linawashikilia watuhumiwa Geofrey Braiton (29) na Michael Ruben (30) wakazi wa jijini humo kwa tuhuma za kupatikana na noti bandia za Sh10,000.

Pia, Jeshi hilo linamshikilia Consolata Mwasege (47) mfanyabiashara mkazi wa Ilomba jijini humo kwa tuhuma za kujihusisha na matukio ya kughushi nyaraka mbalimbali.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi Machi 6, 2025 Kaimu Kamanda wa jeshi hilo, ACP Wilbert Siwa amesema watuhumiwa wa noti bandia walikamatwa wakiwa nyumba ya kulala wageni, katika mtaa na Kata ya Itewe wilayani Chunya.

Amesema watuhumiwa hao walikutwa na noti 15 za Sh10,000 kila mmoja ambapo kama zingekuwa halali ni sawa na Sh150,000 zote zikiwa na namba CA 3903666.

“Lakini pia katika kipindi cha  Februari, jumla ya watuhumiwa 22 walikamatwa wakiwa na dawa za kulevya aina ya bangi kilogram 173.5 na watuhumiwa 14 walikamatwa wakiwa na pombe ya  moshi, maarufu gongo lita 68,” amesema.

“Katika tukio lingine Jeshi la Polisi linamshikilia Consolata kwa tuhuma za kujihusisha na matukio ya kughushi nyaraka, ikiwamo vitambulisho vya Taifa  22 vya   watu tofauti, kadi nne za mpiga kura, vipeperushi vya matangazo ya freemason 200 na kompyuta moja ya kutengenezea nyaraka hizo,” amesema Siwa.

Kamanda huyo amesema mtuhumiwa huyo amekuwa akighushi nyaraka hizo kwa lengo la kujipatia kipato isivyo halali na nyaraka hizo zimepelekwa makao makuu ya Nida.  Dar es Salaam kwa ajili ya uchunguzi.

Amesema Jeshi la Polisi mkoani humo katika kudhibiti ajali na kusimamia sheria za usalama barabarani, wamechukua hatua mbalimbali kwa madereva wasiotii sheria na kusababisha ajali.

“Kwa Februari, madereva saba wamefungiwa leseni kutokana na uzembe na kuhatarisha usalama wa watumiaji barabara, wengine kusababisha ajali, majeruhi na vifo na kesi 13 zimefikishwa mahakamani na washtakiwa kutakiwa kulipa faini,” amesema Kamanda huyo.

Mmoja wa wananchi katika Mtaa wa Sokoine jijini Mbeya, Yesaya Mwakyusa amesema pamoja na adhabu kwa madereva hao, lakini bado miundombinu ya barabara katika mkoa huo si salama akiomba Jeshi la Polisi kuongeza umakini katika kudhibiti mwendo kasi.

“Hiyo inaweza kusaidia madereva wengine kuendesha kwa usahihi, lakini kwa ujumla barabara zetu za Mbeya siyo nzuri, haya matukio yanaweza kuisha au kupungua baada ya njia nne kukamilika,” amesema .