Wawili wakutwa na vimelea vya kipindupindu Bukoba

Bukoba. Watu wawili kati ya watano waliofikishwa katika Hospitali ya Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera wakihisiwa kuwa na dalili za kipindupindu, wamethibitika kuwa na vimelewa vya ugonjwa huo.

Mganga Mkuu wa Hospitali ya Manispaa ya Bukoba, Dk Peter Mkenda amethibitisha hayo leo Januari 31, 2025, alipozungumza na Mwananchi.

Dk Mkenda amesema watu watano, wakazi wa Mtaa wa Matopeni, walioripotiwa na Mwenyekiti wa mtaa huo, Prosper Kyaruzi wakihisiwa kuwa na tatizo hilo na baada ya kuwafikisha hospitalini hapo kufanyiwa vipimo, wawili wamebainika kuwa na vimelea hivyo.

“Naomba wananchi waendelee kuchukua tahadhari kwa kufuata maelekezo tunayowapatia kupitia kwa maofisa afya,” amesema Dk Mkenda.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Matopeni, Kyaruzi amesema Januari 29, 2025, alipata taarifa kuwa mtu mmoja amepelekwa hospitali akiwa anaharisha na alipofanya ufuatiliaji alibaini zipo familia zaidi ya tatu ambazo zilikuwa na tatizo kama hilo.

“Nilitoa taarifa katika Kituo cha Afya Kashai na wataalamu afya walikuja na kawachukua kwa ajili ya kuwafanyia vipimo na baada ya hapo nikatoa taarifa kwa kamati ya usalama, ndo maana mkuu wa wilaya na viongozi walikuja na kufanya kikao,” amesema Kyaruzi.

Mkazi wa mtaa huo, Richard Joakim amesema kuna haja ya kuendelea kuelimisha jamii kuhusu suala la kutumia majisafi na yaliochemshwa kwa shughuli mbalimbali.

“Idara ya afya na maji inatakiwa kutoa elimu kuhusu madhara ya maji machafu tunayotumia kutoka kwenye mito ya Kikaranga, Matopeni na Ziwa Victoria, maana unaweza kumaliza mwezi Bibi afya hajafika kwako,” amesema Joakimu

Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Erasto Sima amesema Januari 30, 2025 alifanya mkutano wa dharura kwenye mtaa huo kuhamasisha jamii kufanya usafi wa mazingira na kuepukana na dhana ya kutumia maji ya mito kwa matumizi ya nyumbani.