
Dar es Salaam. Chama cha Skauti Tanzania kimewafuta uanachama wakufunzi wake wawili, Faustine Magige na Festo Mazengo, kwa tuhuma za kukiuka katiba na sera za chama hicho, ikiwemo ubadhirifu wa fedha zinazohusiana na safari ya kimataifa ya watoto wa skauti.
Taarifa hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa Bodi ya Skauti Tanzania, Rashid Mchatta, leo Jumatano, Mei 7, 2025, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika makao makuu ya chama hicho, Fire, jijini Dar es Salaam.
Mchatta amesema uamuzi huo umetokana na kikao cha Bodi kilichofanyika Februari 27, 2025, kufuatia maagizo ya mkutano mkuu uliofanyika Desemba 14, 2024.
“Mnamo Desemba 11, 2023 tulipokea malalamiko kutoka kwa wazazi kuhusu safari ya watoto 12 kutoka Shule ya Msingi IVY, Kigamboni kwenda Afrika Kusini kushindwa kufanyika. Malalamiko hayo yalihusu utaratibu wa kifedha na mgogoro wa uratibu wa safari,” amesema Mchatta.
Amefafanua Magige alikusanya Sh4 milioni kutoka kwa kila mzazi kwa ajili ya safari hiyo, fedha ambazo aliziingiza kwenye akaunti yake binafsi ya benki kinyume na taratibu za chama.
“Magige ndiye aliyeratibu safari hiyo pasipo kufuata utaratibu wa Skauti. Mwisho wa siku, safari haikufanyika, watoto hawakusafiri na wazazi wakaanza kudai kurejeshewa fedha zao jambo ambalo halikutekelezwa,” amesema Mchatta.
Kwa mujibu wa chama hicho, Januari 1, 2024, kilipokea barua kutoka uongozi wa shule hiyo yenye kichwa cha habari “Udanganyifu uliofanywa na Faustine Magige katika kuratibu safari ya Afrika Kusini.”
Taarifa hiyo ilisababisha kikao cha kamati tendaji kufanyika Januari 20, 2024 na baadaye kamati ya usuluhishi na maadili kusikiliza pande husika Februari 13. Hatimaye, Machi 8, 2025, Bodi ya Skauti Taifa ilikutana na kumpa nafasi Magige kutoa maelezo yake mbele ya bodi.
Magige ajitetea, adai kuonewa
Akijibu tuhuma hizo, Magige amekanusha madai yote, akidai fedha hizo hazikutafunwa naye bali na baadhi ya viongozi wa juu wa skauti waliotofautiana naye kwa sababu za kiutawala.
“Hakuna hela ya maskini niliyokula. Hizi ni njama za viongozi wakubwa walioniandama kwa sababu za kisiasa ndani ya chama. Safari hiyo haikufanyika kwa sababu ya migogoro ya kiuongozi,” amesema Magige.
Aidha, ameeleza utaratibu wa kuweka fedha kwenye akaunti yake binafsi ulikuwa unafahamika kwa baadhi ya viongozi wa juu waliomruhusu kufanya hivyo kabla ya utaratibu mpya wa ukusanyaji fedha kutangazwa.
“Skauti ni taasisi ya maadili, lakini kinachofanyika sasa ni uhuni. Kamati iliyonipitia haikutumwa na waziri, bali ilikuwa ni kundi la watu walioletwa kunitisha na kusema wametumwa na Waziri wa Elimu,” amesema Magige.
Kwa upande wake Festo Mazengo, amesema anashangaa kuona Skauti wanamfuta uanachama wakati jambo bado lipo mahakamani halijatolewa maamuzi bado.
“Hii taarifa ya sisi kuchukua hela kutoka kwa familia maskini sio kweli, kwanza kesi bado lipo mahakamani na tunaitwa pande zote tatu yaani sisi, wazazi na skauti na mara mwisho kwenda mahakamani ni Aprili 25, 2025 pia tumepengawa tarehe nyingine kwenda kusikilizwa kesi yetu, nashangaa leo skauti wanatoa uamuzi kama huo,” amesema Mazengo
Chama chasisitiza uwazi na uadilifu
Kwa upande wake, Chama cha Skauti kimesisitiza dhamira yake ya kuendeleza misingi ya uadilifu, uwazi na heshima kwa wanachama wake, na kuhakikisha haki na taratibu za kisheria zinafuatwa kikamilifu.
“Kuanzia sasa, safari zote za nje ya nchi zitaratibiwa kwa mujibu wa Mwongozo wa Safari za Nje wa mwaka 2024 ambao umeshafikishwa kwa makamishna wa skauti ngazi za mikoa na wilaya,” ilisema taarifa ya chama hicho.