Wawili wafariki dunia ajali Handeni, yumo askari JWTZ

Handeni. Watu wawili wamefariki dunia katika ajali ya gari iliyohusisha Toyota Noah kuigonga Toyota Canter ambayo ilikuwa pembeni ya barabara usiku wa kuamkia leo Jumatatu Februari 10, 2025 eneo la Kauzeni, Kata ya Kwenjugo wilayani Handeni, Mkoa wa Tanga.

Mkuu wa Wilaya ya Handeni (DC), Albert Msando kupitia taarifa yake kwa umma aliyoitoa kupita makundi ya kijamii ya WhatsApp imewataja waliofariki dunia ni Abdul Kareem Kimemeneke (49) ambaye ni askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), kikosi cha 83 Vigwaza.

Askari huyo ni makazi wa Kwamfuko, Kata ya Vibaoni Handeni. Mwingine aliyefariki dunia papo hapo ni mfanyabiashara wa Soko la Chogo, Mussa Juma Athumani (24), mkazi wa Mtaa wa Kwamneke, Kata ya Mlimani, Handeni.

“Kwa masikitiko makubwa natangaza vifo vya Wanahandeni wenzetu wawili waliofariki kwenye ajali eneo la Kauzeni Kata ya Kwenjugo leo tarehe 9 Februari 2025.

“Wenzetu hawa ni Abdul Kareem Kimemeneke (49) ambaye alikuwa askari wa JWTZ kikosi cha 83 Vigwaza na mkazi wa Kwamfuko Vibaoni, Handeni na wa pili ni Mussa Juma Athumani (24) mkazi wa Kwamneke Mlimani Handeni, Mfanyabiashara Soko la Chogo,” amesema Msando.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga (RPC), Almachius Mchunguzi akizungumza na Mwananchi amesema gari Toyota Noah ilikuwa inatoka barabara ya Korogwe kwenda Handeni ilipofika eneo la Kauzeni ambapo kuna kona, ilimshinda dereva na alikuwa na mwendo mkali hivyo kwenda kuigonga gari aina ya Canter.

Amesema dereva wa Noah amesababisha ajali kwa kuigonga Canter ambapo abira kadhaa walipata majeraha na walipelekwa Hospitali ya Mji Handeni, pamoja na miili ya marehemu kwaajili ya taratibu nyingine.

“Taarifa za awali hii Noah ilikuwa inatoka Korogwe kuelekea Handeni sasa kwenye kona eneo la Kauzeni ilimshinda dereva nadhani alikuwa na mwendo mkali akaenda kuivaa Canter ambayo ilikuwa maeneo hayo pia na kusababisha ajali na kutokea majeruhi na watu wawili kufariki dunia,” amesema Mchunguzi.

Shuhuda wa ajali hiyo ambaye pia ni mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kwedisewa, Omari Kibinda amesema ajali hiyo ilitokea saa 2 usiku na ilikuwa mbaya sana kwa maelezo ya awali taarifa zinaeleza Noa ilikodiwa kusafirisha watu hao ambao wamefariki.

Kuhusu gari aina ya Canter amesema ilikuwa inakwenda Wilaya ya Lushoto eneo la Lukozi na ilibeba wafanyabiashara ambao wanakwenda kufungasha bidhaa mbalimbali kama Nyanya na bidhaa nyingine ila wao hawakupata madhara makubwa.

Marehemu wote wametambuliwa huku baadhi ya majeruhi ambao idadi yao bado haijafahamika wakiendelea kupatiwa matibabu katika hospitali ya Mji Handeni.