
MKURUGENZI wa Ufundi wa Mchenga Stars, Mohamed Yusuph amesema timu hiyo itawakosa nyota wake wawili, Jordan Manang na Steve Oguto wanaojindaa kusepa klabuni hapo.
Mchenga inajiandaa na Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BDL) pamoja na timu nyingine na kwa sasa zinafanya usajili kuimarisha vikosi vyao.
Yusuph aliliambia Mwanaspoti, wachezaji hao wanatarajia kutimkia katika moja kati ya zitakazoshiriki ligi hiyo, lakini wamejipanga kuziba nafasi zao kwa kusajili nyota kutoka timu nyingine na hivyo kuwatoa wasiwasi mashabiki wa Mchenga.
“Tutaziba nafasi hizo kwa kusajiji pia baadhi ya wachezaji kutoka nje ya nchi na wachezaji hao tutawatangaza baada ya kuanza mazoezi rasmi,” alisema Yusuph na kuongeza kuhusu mazoezi ya timu hiyo wamepanga kuanza Machi mwaka huu katika Uwanja wa Spide chini ya Kocha mkuu, Mariam Kiwelo.
Yusuph aliyewahi kuichezea Savio miaka ya nyuma nafasi ya pointi guard (namba 1) alisema mipango waliyonayo kwa sasa ni kubeba ubingwa wa BDL.
Mchenga Stars ilitolewa na JKT katika hatua ya robo fainali ikifungwa michezo 3-1.
“Kama tulitolewa kwa bahati mbaya na JKT na timu hiyo ikawa bingwa kwa nini na sisi tusichukue,” alihoji Yusuph, huku akiipongeza Kangaroo Insurance Brokers na mwenyekiti wao Ivan Tarimo kwa kuisapoti timu hiyo katika ligi ya mwaka jana.