Wawili kortini wakidaiwa kusafirisha dawa za kulevya kilo 62

Dar es Salaam. Wafanyabiashara wawili, Quizbat Shirima (38) na Linda Massawe (28) wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na mashtaka mawili likiwemo la kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroine zenye uzito wa kilo 62.298.

Watuhumiwa hao wote ni wakazi wa Dar es Salaam, Shirima (Kibada-Kigamboni) na Massawe (Kimara Bucha-Ubungo),  wamefikishwa mahakamani hapo Ijumaa jioni Februari 14, 2025 na kusomewa kesi ya Uhujumu Uchumi namba 4004 ya mwaka 2025.

Washtakiwa hao wamesomewa mashtaka yao na wakili wa Serikali, Cathbert Mbilingi mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Anna Magutu.

Kabla ya kusomewa mashtaka hao, hakimu Magutu aliwaambia washtakiwa hawatakiwi kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi za uhujumu uchumi.

Pia, hakimu Magutu alisema kiasi cha dawa walichoshtakiwa nacho hakina dhamana kwa mujibu wa sheria.

Akiwasomea shtaka mashtaka yao, wakili wa Serikali Mbilingi alidai kuwa washtakiwa hao wamesafirisha dawa hizo kinyume na kifungu cha 15A (1) na (2) C cha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya sura 95 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Mbilingi alidai June 9, 2023 eneo la Kibada, washtakiwa walikutwa wakisafirisha dawa za kulevya aina ya heroine zenye uzito wa kilo 62. 298 kinyume cha sheria.

Shtaka la pili, siku na eneo hilo, washtakiwa walikutwa wakisafirisha dawa za kulevya aina ya bangi zenye uzito wa gramu 231.31, kinyume cha sheria.

Washtakiwa baada ya kusomewa mashtaka yao, upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na kwamba wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kuwasomea Maelezo ya Mashahidi na Vielelezo (Commital Proceedings).

Hakimu Magutu aliahirisha kesi hiyo hadi Februari 27, 2025 kwa ajili ya washtakiwa kusomewa maelezo yao na ya mashahidi.