Wawili akiwamo mwanahabari wafariki dunia kwa ajali

Ruangwa. Watu wawili wamefariki dunia akiwamo mwandishi wa habari wa Radio Ruangwa na wanne kujeruhiwa katika ajali ya pikipiki iliyotokea wilayani hapa Mkoa wa Lindi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Jumatatu Machi 3, 2025 na Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi, Mkoa wa Lindi Andrea Ngasa, tukio hilo limetokea saa nane usiku wa Machi 1, 2025 katika Kijiji cha Mitope wilayani Ruangwa.

Kamanda Ngasa amesema, ajali hiyo imehusisha pikipiki mbili moja aina ya TVS mali ya Ruangwa FM iliyokuwa ikiendeshwa na Fabian Lupenu (35) na pikipiki nyingine aina ya Haojue iliyokuwa ikiendeshwa na Juma Kasian (28), ambazo ziligongana.

Taarifa hiyo imewataja waliofariki dunia ni Fabian Lupenu na Juma Kasian.

Waliojeruhiwa kwenye ajali hiyo ni Hassan Mguwale (19), Selemani Issa (21), Buruan Said (25) pamoja na Mwamin Beli (34) ambao wamelazwa Hospitali ya Nkowe na Hospitali ya Ndanda kwa matibabu zaidi.

Daktari Alvira Jeremiah wa Kituo cha Afya Nkowe amesema amepokea miili ya Lupenu na Kasian akisema vifo vyao vimetokana na kupoteza damu nyingi baada ya kujeruhiwa vibaya kichwani.

Ziada Juma, ndugu wa Lupenu amesema: “Ukweli ni kwamba pengo la Fabian halitaweza kufutika, tulimzoe sana kwa upendo wake, ucheshi pamoja na ushirikiano kwa majirani zake, msiba huu ni mkubwa sana kwetu.”

Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari ya Lindi (LPC), Fatuma Maumba amesema marehemu alikuwa mwanachama wa LPC mwenye kupenda ushirikiano kwa waandishi wenziwe na hata ambao sio waandishi.

“Tumepata pigo kubwa sana sisi waandishi wa habari wa Mkoa wa Lindi, tumempoteza kijana mchapakazi na mpenda watu, sisi waandishi tunamuombea mwenzetu apumzike kwa amani,” amesema Maumba.