Wawekezaji 200 kutoka nchi 15 kutafuta fursa Tanzania

Dar es Salaam. Ujumbe wa wawekezaji 200 kutoka nchi 15 duniani unatarajiwa kufika Tanzania kuangalia fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo nchini katika sekta mbalimbali ikiwemo uchumi wa buluu.

Ujumbe huo utakuwa jijini Dar es Salaam, Mei 19 na Zanzibar Mei 20 mwaka huu kabla ya kwenda Kampala nchini Uganda kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Jumatatu ya Mei 19, 2025 kwa waandishi wa habari.

Ujumbe huo utaratibiwa kwa ushirikiano wa Benki ya Equity Tanzania na Benki ya Equity Uganda unaendeleza dhamira ya Equity Group ya kubadilisha maisha na vipato kwa kuwaunganisha watu, mitaji na fursa kote Afrika.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Equity Group, Dk James Mwangi linalokwenda kufanyika ni juhudi za kimkakati kufungua fursa zilizopo Tanzania na Uganda kwa kuunganisha mitaji ya kimataifa na fursa za ndani.

“Lengo letu ni kuchochea uwekezaji na biashara zitakazokuwa na athari endelevu kwa kuunda ajira, kuimarisha minyororo ya thamani na kuchangia ukuaji wa uchumi jumuishi,” amesema Dk Mwangi.

Amesema ujumbe huo utakaopita Dar es Salaam, Zanzibar na baadaye Kampala unalenga kuendeleza biashara na uwekezaji wa mipakani na kuimarisha minyororo ya thamani ya kikanda chini ya Mpango wa Afrika wa Urejeshaji na Uhimilivu (ARRP).

Ndani yake utajumuisha wajasiriamali, kampuni za uwekezaji binafsi, washirika wa maendeleo, na wawekezaji wataasisi huku washiriki wakiwa na nafasi kushiriki mijadala ya kitaalamu, mikutano ya biashara (B2B), majukwaa ya Serikali na sekta binafsi.

Pia kutakuwa na ziara za kimkakati katika sekta kama vile kilimo biashara, nishati, utalii, miundombinu, huduma za kifedha, viwanda, na uchumi wa buluu.

Kwa mujibu wake, watakapokuwa Tanzania, wataangazia sekta kuu kama vile usindikaji wa mazao ya kilimo, utalii na hoteli, nishati jadidifu, madini, ujenzi na Tehama.

“Wawekezaji wataangalia maendeleo mbalimbali na fursa zilizopo, ikiwa ni pamoja na uchumi wa buluu wa Zanzibar, miradi ya nishati ya kijani, na uwekezaji wa sekta ya ardhi na makazi,” amesema Dk Mwangi.

Mkurugenzi Mtendaji, Equity Bank Tanzania Mpango mkakati wa benki (ARRP), Isabela Maganga amesema Tanzania inatoa fursa ya kipekee kwa wawekezaji kutokana na kuwa katika masoko ya kikanda.

“Pia ina idadi ya watu inayokua kwa kasi na uwezo mkubwa katika sekta mbalimbali. Msafara huu ni jukwaa la kuiweka Tanzania kama kiungo muhimu katika minyororo ya usambazaji ya kikanda na kimataifa,” amesema Isabela.

Kwa mujibu wake, misafara kama hii imewezesha uwekezaji wa mitaji mikubwa, kuanzisha ushirikiano mpya wa kibiashara na kusaidia kuimarisha ushirikiano wa kibiashara wa kikanda ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa Mkataba wa Biashara Huria wa Afrika (AfCFTA) ambao Equity Group ni miongoni mwa wanaouunga mkono.

Kupitia Mpango wa Afrika wa Urejeshaji na Uhimilivu, Equity Group inarejesha mtaji wa kiwango cha hadi asilimia mbili ya Pato la Taifa (GDP) wa ukanda huu kwenda sekta binafsi, ikilenga minyororo muhimu ya thamani katika kilimo, viwanda, biashara ndogo na za kati (MSMEs), na miundombinu.

Mpango huu unalenga kuwafikia watu na biashara milioni 100 ifikapo mwaka 2030, na kuunda hadi ajira milioni 50 kote barani Afrika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *