
Unguja. Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wamesema kuwa licha ya kuongezeka kwa idadi ya watalii nchini, bado hakuna mkakati madhubuti wa kuwezesha watalii wa ndani kunufaika na vivutio vya utalii, kutokana na gharama kubwa zinazowalenga zaidi wageni kutoka nje ya nchi.
Kwa mujibu wa Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale, kumekuwa na ongezeko kubwa la watalii wanaoingia nchini kila mwaka, kutoka watalii 260,644 mwaka 2020 hadi kufikia watalii 737,775 mwaka 2024, sawa na ongezeko la asilimia 65.
Aidha, idadi ya watalii walioingia mwaka 2024 pekee imeongezeka kwa asilimia 15, kutoka watalii 638,498 mwaka 2023 hadi 736,755 mwaka 2024.
Hata hivyo, takwimu hizo hazijabainisha wazi uwiano kati ya wageni wa kimataifa na watalii wa ndani, jambo ambalo limezua mjadala miongoni mwa wajumbe.
Wakizungumza leo, Mei 20, 2025, wakati wa kuchangia hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale barazani Chukwani, Zanzibar, baadhi ya wajumbe walieleza kusikitishwa na ukosefu wa mkakati wa kuwawezesha wananchi wa ndani, hususan vijana na wanafunzi kutembelea maeneo ya kihistoria na vivutio vya utalii kwa gharama nafuu.
Mwakilishi wa Mtambwe, Profesa Omar Fakih Hamad amesema kuwa Serikali haijaweka mwongozo au mpango mahususi wa kukuza utalii wa ndani, ambao mbali na kuchochea elimu na utambuzi wa urithi wa kihistoria, pia ungeweza kuongeza mapato ya Taifa kupitia ushiriki wa wananchi katika sekta hiyo.
“Hatuwezi kuitegemea tu soko la watalii kutoka nje. Ni muhimu kuweka sera itakayorahisisha upatikanaji wa huduma za utalii kwa wananchi wa kawaida, wakiwemo wanafunzi, ili kuhamasisha uzalendo na kufungua fursa zaidi za kiuchumi ndani ya nchi,” amesema Profesa Hamad.
“Bado kama nchi hatujawa na mpango madhubuti au mwongozo wa kuimarisha utalii wa ndani. Kuna haja sasa ya Serikali kuja na mkakati maalumu utakaowawezesha wananchi kunufaika na sekta hii muhimu, sambamba na kuongeza pato la Taifa,” amesema.
Akifafanua zaidi, amesema kuwa licha ya kuongezeka kwa idadi ya hoteli na miundombinu ya utalii, huduma nyingi bado hazimlengi mtalii wa ndani, kwani gharama ni kubwa na ngumu kumudu kwa wananchi wa kawaida.
Amesisitiza kuwa ipo haja ya kuwa na utaratibu wa kuwezesha na kuhamasisha ushiriki wa Watanzania katika utalii wa ndani kwa kuweka bei rafiki na vivutio vinavyopatikana kwa urahisi.
“Gharama zilizopo sasa ni kubwa mno kwa wananchi wa ndani. Ni wakati muafaka sasa kwa Serikali kuharakisha uboreshaji wa mazingira ya utalii wa ndani, ili kuongeza ushiriki wa Watanzania wenyewe,” ameongeza.
Aidha, amesema changamoto hiyo imechangiwa pia na ukosefu wa mkakati wa kuimarisha maeneo ya kihistoria, pamoja na kutokuwepo kwa msukumo wa masomo ya historia katika shule na vyuo, hali inayowafanya wananchi wengi kutoona umuhimu wa kutembelea maeneo ya urithi wa kitaifa, na hivyo kuwaachia wageni pekee jukumu hilo.
“Tunapaswa kuwekeza kwenye historia yetu kwa kuiboresha, kuihifadhi na kuifundisha ipasavyo. Hatuwezi kuendelea kutegemea wageni pekee kutambua thamani ya urithi wetu,” amesema.
Amesema baadhi ya maeneo ya kihistoria ni kama vichakani kwa hiyo kukosekana kwa haiba nzuri nako kunashusha hadhi ya maeneo hayo.
Mwakilishi nafasi za wanawake, Chumu Kombo Khamis amesema ni muhimu kuwekeza katika utalii wa ndani kama wanavyofanya China kwani asilimia kubwa ya wageni wanakuwa ni watalii wa ndani.
Amesema wamefikia huko kwa sababu wameboresha mazingira na kuweka mazingira rahisi kwa ajili ya wazawa kutembelea vivutio na uhamasishaji unaofanywa na Serikali na wadau wengine.
“Serikali ikiweka mazingira mazuri na wananchi wakahamasika kushiriki kutembelea maeneo ya ndani badala ya kusubiri wageni kutoka nje ya nchi, kama inavyofanya China,” amesema.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mfenesini, Machano Othman Said amesema ni vyema wizara ikashiriki mikutano mikubwa ya kimataifa ili kuitangaza Zanzibar na kuvutia wageni wengi zaidi.
Hoja hiyo imeungwa mkono na mwakilishi wa kuteuliwa na Rais, Juma Ali Khatibu (Ada Tadea) akisema kuwe na mpango maalumu wa maonyesho hata ya ndani ambayo inakuwa fursa nzuri katika kukuza utalii.
Naye Mwakilishi wa Mtoni, Hussein Ibrahim Makungu amesema bado Serikali kupitia wizara hiyo inapoteza mapato kwa sababu ya kutokuwapo kwa mifumo ya kufuatilia wageni tangu wanapoingia ndani ya nchi na wanapokwenda.
Kauli hiyo, hata kwenye bajeti ya wizara ilikiri kupotea baadhi ya mapato katika maeneo ya kihistoria kutokana na kutokuwapo kwa baadhi ya watendaji ambao sio waaminifu na kuchukua fedha hizo.
“Hili nimewahi kusema hata mwaka jana hapa barazani, mapato mengi yanapotea lazima kuwe na mfumo mmoja wizara, kamisheni ya utalii, Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA) na Uhamiaji wawe na mfumo mmoja kufuatilia wageni tangu wanapoingia nchini hadi wanapokwenda kulala na siku wanazotumia,” amesema.
Naibu Spika, Mgeni Hassan Juma amesema wizara iendelee kutangaza visiwa ili kukuza pato kupitia sekta ya utalii, huku akiitaka kuwainua wawekezaji wa ndani badala ya kutegemea wa kutoka nje ya nchi.
Baraza limejadili na kuipitisha bajeti wizara hiyo ya Sh45.032 bilioni kwa ajili ya kutekeleza vipaumbele 10 kwa mwaka wa fedha 2025/26.