Wawakilishi walalama kesi za udhalilishaji kuja kivingine

Unguja. Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wameitaka Serikali kufanya mapitio ya Sheria ya Mtoto, wakieleza kuwa kumeibuka changamoto ya madai ya kubakwa ambayo wakati mwingine yanaibuliwa na watu wanaodaiwa kuwa watoto, ilhali wao wenyewe ndio hujihusisha na masuala ya mapenzi.

Aidha, wawakilishi hao wametoa wito kwa Serikali kuweka mkazo zaidi katika elimu ya malezi, wakibainisha kuwa wazazi wengi wa kizazi cha sasa wamesahau majukumu yao ya msingi na kuwaachia watoto uhuru usio na mipaka, hali inayochangia kuongezeka kwa matukio ya udhalilishaji na mmomonyoko wa maadili.

Hayo yameelezwa leo, Mei 15, 2025, wakati wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wakichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

Mwakilishi wa Ziwani (CCM), Suleiman Makame Ali, amesema kuna haja ya kufafanua kwa uwazi zaidi umri wa mtoto kisheria, kwani hali halisi mitaani inazua maswali mengi tangu kupitishwa kwa Sheria ya Udhalilishaji.

Amesema mara nyingi waathirika wa sheria hiyo wamekuwa ni watoto wa kiume, jambo linalopaswa kuangaliwa kwa makini ili kuepusha madhara yasiyo ya lazima kwa kundi hilo.

Mwakilishi huyo amesema ukiendelea utaratibu kama ulivyo sasa vijana wataishia jela kwa kusingiziwa kubaka na kudhalilisha, ilhali wengine wanakubaliana.

“Haiwezekani mtu apande magari matatu anakwenda kwa mwanaume halafu tuje tuseme huyo kabakwa, huu ni mpango watu wamegeuza kama biashara kisha udhalilishaji.

“Hili jambo linaumiza wengi hawa wote ni watoto wetu, wa kike na kiume, lakini kuna changamoto kubwa watu wanatumia vibaya nafasi hiyo, kwa hiyo leteni sheria hapa kwanza tujue mtoto ni yupi ila tukiliacha liende hivi hali itakuwa hatari,” amesema. 

Aidha, Mwakilishi wa Ziwani (CCM), Suleiman Makame Ali, ameeleza kushangazwa na kushuka kwa bajeti ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kutoka Sh23 bilioni mwaka wa fedha 2024/25 hadi Sh17 bilioni kwa mwaka wa fedha 2025/26, licha ya programu kubakia zilezile.

Ameitaka Serikali kufafanua sababu za kupunguzwa kwa bajeti hiyo.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Viti Maalum, Mwachumu Khamis amesema ongezeko la talaka ni miongoni mwa changamoto kubwa zinazolikumba jamii, akibainisha kuwa vijana wengi huingia kwenye ndoa bila uelewa wa kina juu ya misingi yake, hali inayosababisha kuvunjika mapema na watoto kukosa malezi bora.

“Kuna uwajibikaji mdogo katika malezi. Wazazi wengi wamewaachia watoto kujilea wenyewe. Kuzaa ni jambo moja, lakini kulea ni jambo jingine. Wazazi wengi wameacha utamaduni wa malezi, jambo ambalo linachangia ongezeko la matatizo katika jamii,” amesema Mwachumu.

 “Mafunzo ya ndoa bado ni muhimu sana kwa mazingira ya sasa. Vijana hawaandaliwi ipasavyo kwa maisha ya ndoa. Kama malezi yamelegea, basi hata wanapoingia kwenye ndoa hukosa msingi imara, hivyo kuwapo kwa migogoro inayovunja ndoa,” ameongeza.

Mwakilishi wa Mtoni (CCM), Hussein Ibrahim Makungu, amesisitiza kuwa ingawa Wizara inaweza kupambana na changamoto zinazojitokeza, bila kurejea nyuma na kutathmini misingi ya malezi, hali hiyo itaendelea kutokea.

Makungu amesema kuwa si vyema kuendelea kujadili masuala ya talaka bila kuchukua hatua madhubuti, akiongeza kwamba ni muhimu ofisi husika zichukue jukumu la kutoa elimu ya ndoa kwa wanandoa, kwani ongezeko la talaka linazidi kuwa tatizo kubwa.

Kwa upande mwingine, Mwakilishi wa Viti Maalumu, Shadya Mohamed Suleiman amesema mifarakano ya ndoa ni miongoni mwa sababu kuu za ukatili katika jamii, na hivyo ni lazima kuweka mipango kabambe ya kuziimalisha ili kuzuia vitendo vya ukatili.

Awali, akiwasilisha bajeti ya Wizara hiyo, Waziri Riziki Pemba Juma amesema kuwa inatekeleza vipaumbele 11 na aliomba Baraza la Wawakilishi liidhinishe Sh17.072 bilioni kwa ajili ya utekelezaji wa vipaumbele hivyo.

Waziri Riziki alisema vipaumbele hivyo vitajikita katika kuimarisha huduma za malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya watoto katika familia, jamii na taasisi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *