Serikali mkoani Mara imeitaka Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Rorya kufanya tathmini ya haraka baada ya wavuvi katika Ziwa Victoria humo kulalamika wanavamiwa na kuibiwa kila wanapokuwa majini na watu kutoka nchi za jirani.
Ziwa Victoria linamilikiwa na nchi tatu za Tanzania, inayolimiliki kwa asilimia 51, Uganda asilimia 43, na Kenya ikiwa na asilimia sita.
Februari 7, mwaka huu, Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Stephen Wasira, aliwataka wavuvi wanaofanya shughuli zao ndani ya Ziwa Victoria kuchukua tahadhari na kuepuka kuvuka mipaka ya nchi nyingine ili kujiepusha na matatizo yasiyo ya lazima.
Wasira alitoa tahadhari hiyo baada ya kupokea taarifa kuwa, ndani ya miezi mitatu, wavuvi zaidi ya 12 walivamiwa na kuporwa samaki na zana zao za uvuvi.
Jana, Februari 28, 2025, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Evans Mtambi, alisikiliza kero na changamoto za wakazi wa Kijiji cha Komuge wilayani Rorya, ambapo baadhi ya wavuvi walidai kuwa uvamizi huu umeongezeka kwa kasi zaidi.
Walisema wavuvi wanavamiwa kila siku na kwamba askari wanaoendesha doria pia wanashirikiana na wahalifu kutoka nchi jirani zinazopakana na Ziwa Victoria.
Mvuvi Charles Shishi, amesema vitendo hivi vya uvamizi vimeongezeka kwa kasi, na wavuvi hawajui cha kufanya.
Ameomba Serikali ichukue hatua haraka kudhibiti wimbi hili la uvamizi ili kuwanusuru.
“Sasa hivi vitendo vinatokea kila siku. Wavuvi tunavamiwa na maharamia kutoka nchi za jirani, wengine wakiwa na boti zenye namba za usajili za nchi zao, na wengine hawana namba za usajili. Tunaomba Serikali itusaidie kwani hali hii inatuathiri sana,” amesema Shishi.

Shishi ameeleza kuwa yeye binafsi amekutana na tukio hili mara kadhaa ambapo alinyang’anywa samaki pamoja na mafuta ya petroli aliyokuwa akitumia kwa mashine yake, na alikolewa na wavuvi wenzake baada ya kukaa ziwani kwa saa kadhaa.
Magesa Ezekiel ameeleza kuwa hivi karibuni kijana mmoja alijeruhiwa kwa kupigwa risasi mguuni baada ya kujaribu kuwazuia maharamia kuchukua samaki, na baada ya kujeruhiwa, maharamia hao walitokomea na samaki.
Amesema mbali na kuhatarisha usalama wao, vitendo hivyo vinadhoofisha utendaji wao wa kazi na kuwarudisha nyuma kimaendeleo.
Baada ya kusikiliza kero hizo, Mtambi ameagiza Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Rorya kufanya tathmini ya haraka kuhusiana na suala hili na pia kuweka mikakati ya kupambana nalo.
“Mkoa tunalichukua suala hili kulifanyia kazi kwa umuhimu na unyeti wake, lakini wakati huo DC na kamati yako kaeni mfanye tathmini ya hali halisi na kuangalia mna uwezo kiasi gani. Pia, tunaishukuru Serikali kwa kuongeza mafuta kwa ajili ya doria,” amesema Mtambi.
Mtambi amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Rorya kufanya vikao vya ujirani mwema na wakuu wa wilaya za nchi jirani ili kujadili suala hili, akisisitiza kuwa usalama wa raia ni jambo la msingi.
Pia, amezungumzia tuhuma za baadhi ya wavuvi wa Tanzania na askari wanaoendesha doria kushirikiana na maharamia kutoka nchi jirani, akisema suala hilo litafanyiwa kazi kwa haraka ili hatua stahiki zichukuliwe.
“Hili jambo ni nyeti kwani linahusu usalama wa watu wetu na mali zao. Awali, ilidaiwa kuwa wavuvi wa huku wanavuka mpaka na kwenda kuvua kwenye maji ya nchi za jirani, lakini hayo madai sasa yanaonekana kuwa hayana uhalisia. Lazima tuchukue hatua za haraka,” alisema Mtambi.
Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Halfan Haule, amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo na kusema kuwa tayari wameanza kuifanyia kazi, huku wakifanya doria za mara mbili kwa wiki.
“Tunashukuru Serikali imetuongezea mafuta kwa ajili ya boti za doria na hivyo sasa tunafanya doria mara mbili kwa wiki,” amesema Haule.