Tanga. Ikiwa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa taarifa kuhusu uwepo wa kimbunga Jude katika Bahari ya Hindi, eneo la Rasi ya Msumbiji, na uwepo wa mvua nchini kwenye baadhi ya mikoa, wavuvi mkoani Tanga wamesema yapo madhara yanayoweza kutokea na kusababisha hasara hasa kwenye shughuli zao.
Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti kuhusu uwepo wa kimbunga Jude na mvua kwa Mkoa wa Tanga leo Machi 12, 2025, wavuvi wadogo wa soko la Samaki la Mwalo wa Deep Sea jijini Tanga wamesema yapo madhara ambayo yanaweza kutokea, hivyo waendelee kupewa taarifa na tahadhari.

Mvuvi wa Mwalo huo wa Deep Sea, Ally Rashid amesema mvua inapokuwa kubwa na upepo baharini kuna uwepo wa giza hali ambayo hata nahodha wa vyombo vya usafiri kushindwa kuona mbele, jambo ambalo linaweza kuwa ni hatari kwa abiria aliowabeba na chombo kwa ujumla.
Madhara mengine samaki wanakuwa hawapatikani kwa kukimbia mawimbi ya mvua na kushuka chini kabisa hali ambayo hakuna mvuvi anaweza kuwafikia, kwani wanazama kwenye kina kirefu kutokana na hali ya hewa kuchafuka.
Ameeleza kitu kingine ni kukiwa na upepo hakuna chombo kinachoweza kuingia baharini, mawimbi ya bahari yanapokuwa makubwa samaki wanakwenda kujificha lakini pia usalama wa wavuvi unakuwa ni mdogo.
“Hali ya hewa inapochafuka baharini kwa uwepo wa Kimbunga au mvua sisi wavuvi hatuna kazi kabisa, samaki hawapatikani na kule tunakokwenda hatuwezi kuona kabisa, kwa maana hiyo hata samaki hawawezi kupatikana haya yote ni madhara ya uwepo wa kimbunga na mvua,” amesema Ally.
Nahodha wa vyombo vya baharini, Salimu Ramadhani amesema zipo hatua za tahadhari ambazo wavuvi wanatakiwa kuzichukua wakikutana na changamoto baharini, ikiwemo kuhakikisha wanaweka nanga, kuwa na kifaa cha kutambua mwelekeo, (GPS).
Amesema bila kuwa na nanga nzuri pamoja na GPS ambayo itasaidia wavuvi kujua mwelekeo wa sehemu wanayotaka kwenda na walipo itawawia ugumu, endapo watakutana na kimbunga au mvua wanapokuwa baharini.
Wanayotakiwa kufanya wavuvi Ofisa Uvuvi halmashauri ya jiji la Tanga katika mwalo wa Deep Sea, Leonard Mwakyusa amesema zipo tahadhari muhimu ambazo wavuvi wote wanatakiwa kuzichukua wanapoingia baharini, ikiwemo kuwa na majaketi ya uokoaji, kuhakikisha vyombo vyao havina tatizo lolote, kubeba vifaa vitakavyowasaidia kuomba msaada endapo watapata dharura.
Amesema wao kama viongozi wanaosimamia sekta hiyo ya uvuvi wanaendelea kutoa elimu ya mara kwa mara kwa wavuvi wao, endapo wakipata taarifa ya kuwepo mvua au majanga kama kimbunga kwani kwa kufanya hivyo inaweza kuwasaidia kujihadhari mapema.
Katibu wa Chama cha Wavuvi Wadogo Tanga, Faki Mbaruku Kombo ameziomba mamlaka zinazofuatilia uwepo wa mabadiliko ya hali ya hewa ikiwemo baharini, kuwa karibu nao kwa kuwapa taarifa mapema zaidi, endapo wataona kuna dalili za kuonekana kimbunga au mvua zinazoweza kuleta madhara kwao.
Hata hivyo Kimbunga Jude hakitarajiwi kuwa na athari za moja kwa moja kwa Tanzania, uwepo wake unatarajiwa kuathiri mifumo ya hali ya hewa nchini, ikisababisha ongezeko la mvua katika maeneo mbalimbali. Hali hii pia inaendana na kuanza kwa msimu wa mvua za Masika 2025, kama ilivyotabiriwa na TMA katika taarifa iliyotolewa Januari 31, 2025.