Waviu 23,850 wabainika kuwa na VVU hatua ya juu

Dar es Salaam. Jumla ya watu 23,850 wanaoishi na VVU (Waviu) walifika katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini wakiwa katika hatua za juu za ugonjwa wa VVU na Ukimwi katika kipindi cha miezi sita, kuanzia Julai hadi Desemba 2024, takwimu za Wizara ya Afya zinaonyesha.

Idadi hiyo ni kati ya watu waliokwenda vituo vya afya vinavyotoa huduma za tiba na matunzo (CTC) na kupimwa kinga ya mwili, ambapo 14,051 walikuwa katika hatua ya tatu na nne ya ugonjwa, huku 9,804 wakiwa na kiwango cha seli za CD4 chini ya 200.

“Katika idadi hii, waviu 47,212 walipimwa CD4 na waviu 34,508 walipimwa HIV WHO Clinical Staging. Kati ya hawa, waviu 9,804 walikuwa na CD4 chini ya 200 na waviu 14,051 walikuwa katika HIV WHO Clinical Staging hatua ya 3 na 4. Hivyo, idadi ya waviu waliokuwa na AHD katika kipindi hiki ni 23,850.”

“Hizi ni takwimu zilizopatikana kupitia Kitengo cha Huduma za Tiba na Matunzo ya Ukimwi (CTC),” amesema Ofisa Mpango, Dk Sylvester Kwilasa.

Dk Kwilasa kutoka Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi, magonjwa ya ngono na homa ya ini (NASHCoP) amesema wizara imekuwa ikihakikisha kuna ufuatiliaji wa wagonjwa wa AHD baada ya matibabu kupitia mfumo wa CTC.

Alipozungumza na Mwananchi mapema mwaka huu, Mratibu wa Kitengo cha Huduma za Tiba na Matunzo ya Ukimwi (CTC) katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Amana, Dk Joshua Kajula, amesema changamoto hiyo huwakumba baadhi ya vijana.

Amesema kuwa, kati ya mwaka 2023 na 2024, wagonjwa 390 walioanza huduma kwenye kitengo hicho waliogunduliwa kuwa na Advanced HIV Disease walikuwa watu wazima 170. Watoto walio chini ya miaka 24 walikuwa 42, huku wagonjwa waliokuwa na ugonjwa huo wakiwa 12.

“Wengi wanajihisi kuwa maambukizi, lakini wanaogopa kupima kujua hali zao kiafya. Anaumwa lakini kwenda kupima anaogopa, hivyo anajikuta anakwenda njia tofauti.

“Mwingine atapita kwa kila aina ya waganga, anatibiwa famasi kwa kununua dawa, na wengine wanakwenda kwa imani za kidini kwa manabii mbalimbali. Wanapoona imeshindikana, analetwa na ndugu. Akifika hospitalini hajiwezi, ndipo tunaanza kumtibu na kuona namna ya kupandisha CD4 zake,” amesema Dk Kajula.

Daktari Kija Kibwana kutoka Hospitali ya Chalinze amesema kwa mwaka 2024, halmashauri hiyo ilibaini wagonjwa watatu waliokuwa na AHD, ambao tayari wameanza kutumia dawa.

 “Kama mpokea huduma anaendelea na tiba, mwanzoni tunampima CD4. Ikiwa kipimo kinaonyesha zaidi ya 350, hapaswi kupima tena kipimo hicho kila baada ya muda. Lakini kama majibu yatakuwa chini ya kiwango hicho, atapimwa kila baada ya miezi sita ili kufuatilia kinga yake ya mwili,” amesema DkKibwana.

Kwa upande wa vijana wenye umri wa miaka 15-24, amesema kuwa wanawahudumia vijana 128 katika kituo hicho, ambapo 48 ni wa kiume na 80 ni wa kike.

Kufuatia hilo, wataalamu wa afya wamesema idadi hiyo ya waviu waliofikia hatua ya juu ya ugonjwa inaonyesha kuwa hakuna mwamko wa kupima maambukizi ya VVU miongoni mwa jamii, hali inayohatarisha afya ya umma na uwepo wa usugu wa dawa za kufubaza makali ya VVU (ARV) miongoni mwa waviu.

Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania MAT, Dk Mugisha Nkoronko amesema:“Hatua hizi za juu zinachangia kuwepo na maambukizi zaidi kwa maana mviu anafikia mpaka hatua ya tatu na nne ya ugonjwa hajabaini ni rahisi kuambukiza wengine.

“Pia inaashiria kwepo kwa unyanyapaa, kutotumia dawa kwa ulinganifu na umbali wa kuzifikia huduma za afya.”

Changamoto na matokeo ya tafiti

Ugonjwa wa VVU hatua ya juu huongeza hatari ya vifo na matatizo mengine ya kiafya. Utafiti uliofanyika katika maeneo ya vijijini Tanzania ulionyesha kuwa, licha ya utekelezaji wa miongozo ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ya Test and Treat, bado kuna mzigo mkubwa wa AHD na vifo vinavyohusiana na hali hiyo.

Licha ya juhudi hizo, bado kuna changamoto katika kugundua na kutibu AHD mapema. Ucheleweshaji wa kugundua VVU na kuanza matibabu huongeza hatari ya mtu kufikia hatua ya AHD.

Utafiti umeonyesha kuwa asilimia 42.4 ya watu wanaogunduliwa na VVU nchini Tanzania wanagunduliwa wakiwa tayari katika hatua ya kuchelewa, na asilimia 17.7 wakiwa katika hatua ya AHD. Kila mwaka, kuna maambukizi mapya takriban 60,000 miongoni mwa watu wenye umri wa miaka 15 na zaidi.

Ufafanuzi na hatua za Serikali

Akizungumzia upatikanaji wa matibabu, Dk Kwilasa amesema waliokutwa na hatua za juu wamekuwa wakipatiwa dawa maalumu zinazopatikana katika vituo vyote vya afya.

“Dawa za Cryptococcus Infection na kifua kikuu zinapatikana katika hospitali na vituo vya afya vya umma. Aidha, dawa za Cryptococcus Meningitis zinapatikana katika hospitali zilizotambulika na kuwa na uwezo wa kutoa huduma hizo,” amesisitiza.

Kuhusu dawa za kinga dhidi ya magonjwa nyemelezi, amesema Serikali imehakikisha upatikanaji wa dawa za Cotrimoxazole na ant-TB (3HR, 3HP, INH) pamoja na utoaji wa huduma hiyo ya tiba kinga (Prophylaxis) katika hospitali na vituo vya afya vya umma.

Alipoulizwa kuhusu maeneo yasiyofikika na iwapo serikali ina mpango wa kupanua upatikanaji wa dawa na vifaa vya uchunguzi wa AHD katika vituo vya afya vya vijijini, Dk Kwilasa amesema;

“Huduma hizi zinapatikana katika vituo vyote vinavyotoa huduma za tiba na matunzo (CTC) kupitia mfumo maalumu. Aidha, Serikali ina mpango wa kuongeza vituo vya AHD hadi ngazi ya hospitali za wilaya zote nchini kufikia Machi 2025,” amesema.

Kuhusu upatikanaji wa huduma za haraka kwa wagonjwa wenye AHD, Dk Kwilasa amesema NASHCoP imekuwa ikichukua hatua kadha wa kadha kuhakikisha huduma za haraka zinapatikana kwenye kundi hilo.

Mojawapo ni kuhakikisha upatikanaji wa vitendanishi vya CD4 kwa ajili ya kuwatambua wavui wenye AHD, upatikani wa vitendanishi vya kupima magonjwa nyemelezi kama Cryptoccocus, kifua kikuu ili kuwatambua.

Pamoja na hayo, Dk Kwilasa amesema Wizara ya Afya imekuwa ikifanya ufuatiliaji wa utekelezaji wa afua ya AHD kupitia taarifa na ripoti za utekelezaji, ili kuhakikisha huduma za haraka zinapatikana kwa wagonjwa waliopo katika hatua hiyo.

Ametaja mikakati ya wizara ikiwa ni pamoja na utoaji wa huduma za AHD kupitia miongozo ya kitaifa iliyoelekeza kwa kina namna ya kutambua, kutibu na kufuatilitia waviu wote wenye AHD katika vituo vya kutolea huduma nchini.

Kuhusu ufadhili na ushirikiano, Dk Kwilasa amesema; “Serikali imekua ikishirikiana na mashirika ya kimataifa kama WHO, PEPFAR na Global Fund katika kupambana na kutoa huduma za AHD kupitia njia mbalimbali kama kufadhili ununuzi wa vitendanishi na dawa, kusaidia utengenezaji wa miongozo na kusaidia kufundisha watoa huduma.

“Mashirika ya kimataifa kupitia wadau wa maendeleo kwa kushirikiana na Serikali wamekuwa wakisimamia utoaji wa huduma za AHD katika Hospitali na vituo vya afya vya umma.”