Wauzaji vileo makazi ya watu watimuliwa, wapewa siku 17 kuhama

Wauzaji vileo makazi ya watu watimuliwa, wapewa siku 17 kuhama

Mbeya. Uongozi wa Serikali ya Mtaa wa Kisunga, Kata ya Mabatini jijiji Mbeya  umefanya operesheni maeneo yanayotajwa kuuzwa pombe haramu ya gongo na kutoa onyo kwa wauzaji wa vileo katika makazi ya watu kufunga biashara hizo.

Hatua hiyo imefanyika kutokana na kukithiri matukio ya uharifu katika Mtaa wa Kisunga Kata ya Mabatini jijini hapa hali inayotajwa kuwa baadhi ya watu wasio na nia njema kutumia maeneo hayo kama vichaka vyao kukaa ili kufanya uhalifu nyakati za usiku.

Uongozi wa Mtaa eneo hilo umetoa onyo, huku ikiwatahadharisha wamiliki wa nyumba walio wapangisha wafanyabiashara pombe haramu ya gongo kusitisha mikataba hadi kufikia Juni 7, 2025.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumanne Mei 20, 2025, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kisunga, Ajuaye Kyando amesema wamefikia hatua hiyo kutokana na kuwepo kwa matukio ya uharifu na kero za muziki ya sauti kubwa nyakati za usiku.

“Tumefikia hatua hiyo kutokana na kuwepo kwa matukio mbalimbali ya uharifu ambao hutumia mwanya wa uwepo wa maeneo ya vilevi kama sehemu ya kujificha na kutekeleza maovu yao,”amesema.

Kyando amesema tayari walifuata utaratibu wa kuwaita baadhi ya wauzaji  wa vileo kwenye ofisini za Serikali ya Mtaa na  kuwaeleza kwa  kuwapa maelekezo sambamba na barua rasmi za kusitisha biashara hiyo haraka iwezekanavyo.

“Tuliwaita ofisini na kuwapa sababu za kupiga marufuku biashara vileo vya kawaida kwenye makazi ya watu na kuwaonya wale wanaodhaniwa kujihusisha na biashara ya gongo,” amesema.

Amesema hatua hiyo ni baada ya kuwepo kwa malalamiko kadhaa ya watu kufanyiwa matukio ya uharifu, yakiwepo ya uvunjaji wa nyumba na kuiba jambo ambalo kama serikali imeona ni vyema kuchukua hatua.

“Sheria haziruhusu biashara za vileo vya aina yoyote katikati ya makazi ya watu, bali yapo maeneo rasmi ambayo hutengwa kwa ajili ya shughuli za pombe na kumbi za starehe,” amesema.

Katika hatua nyingine, Kyando amesema endapo wamiliki wa nyumba watakaidi  kuwaondoa wafanyabiashara wa pombe maeneo ya makazi ya watu, Serikali ya Mtaa imeridhia kuwataka na wao kuhama na badala yake nyumba zao zitumike kupangisha wapangaji wa kawaida.

“Muda tuliotoa ni mrefu, sasa kama mmliki ataona ni vyema wapangaji wake wawe wauzaji wa pombe basi ni vyema naye ahame kwani anakuwa anachochea kuwepo kwa matukio ya uharifu katika jamii,” amesema.

Kuhusu waliofungua maduka ya vileo

Amesema wametoa mwongozo wa kuwataka kubomoa vibanda ambavyo vimejengwa kwenye makazi yao sambamba na kutafuta maeneo rasmi ya kufanyia biashara hizo.

“Tunaposema kuuzia pombe kwenye makazi ya watu haijalishi kama ni  bia na vinginevyo, kwa ujumla tumetoa maelekezo isiwepo sehemu yoyote ya kuuza vinywaji kwenye makazi ya watu ili kulinda usalama wa raia na mali zao sambamba na kuokoa kizazi kijacho kupata haki ya kupata elimu na kuishi mazingira bora,” amesema.

Ameongeza kuwa,”Ifikapo Julai 7, 2025, Mtaa wa Kisunga asiwepo mtu/watu wanaouza pombe aina yoyote kwani itaanza oparesheni maalumu itakayohusisha Jeshi la Polisi kuwakamata wakahidi na kuwachukulia hatua,” amesema.

Kuhusu athari iliyopo

Kyando amesema wanashuhudia watoto wadogo kuacha kuhudhuria masomo na badala yake kusaidiana na wazazi kuuza pombe jambo ambalo ni kuwanyima haki za msingi za  kupata elimu.

“Kuna watoto wanaacha masomo kutokana na wazazi kushindwa kutekeleza majukumu yao na badala yake kuwashirikisha kwenye biashara haramu ya gongo ,ambao pia ufikia wakati kujiingiza kwenye matumizi ya vileo na michezo ya kamali  wakiwa na umri mdogo,” amesema.

Kauli za wafanyabiashara wa vileo

Mmoja wa wauzaji wa vileo, Sikujua John (siyo jina lake halisi), amesema wamepokea maelekezo ya serikali ya mtaa, lakini wanashindwa kuacha kwa kile alichodai biashara hiyo inaendesha maisha yake na kutunza familia.

“Kwa kweli tupo njiapanda hatujui tutafanya nini? Wengi wetu tuna mikopo kausha damu, kwenye taasisi za kifedha na tunategemea marejesho kupata kupitia biashara ya gongo na pombe nyinginezo,” amesema.

Amesema anaomba serikali kuangalia njia mbadala ya kuwasaidia ili wabuni miradi mingine.

Kauli za wananchi

Naye, Alex Kibona Mkazi wa Sabasaba jijini hapa, amesema katazo la uongozi wa Serikali ya Mtaa wa Kisunga Kata ya Mabatini ni sahihi kwa madai vijana wanapoteza nguvu kazi kufuatia muda mwingi kutumbukia kwenye ulevi kutokana na biashara hizo kufanyika maeneo ya makazi ya watu.

“Naunga mkono maamuzi wa serikali kwani mtaa huo ukienda saa 12.00 asubuhi vijana wamelewa pombe na haujulikani wanafanya kazi saa ngapi, lakini tuombe Jeshi la Polisi kufanya oparesheni maalumu,” amesema.

Awali akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga kuhusiana na hatua hiyo ya uongozi wa serikali wa Kisunga amesema atafuatilia, huku akikemea wananchi kujihusisha na biashara haramu za gongo katika Mkoa wa Mbeya.

“Mwandishi ngoja niwasiliane na askari kata nijue kama anayo nakala ya barua kutoka serikali ya mtaa husika kuhusiana na katazo hilo ,huku akibainisha Polisi watafanya doria maeneo mbalimbali hususani kwenye vilabu vya pombe za kienyeji kudhibiti unywaji muda wa kazi,” amesema Kuzaga.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *