Arusha. Siku moja tangu apatikane Mchungaji wa Kanisa la Huduma ya Kristo lililopo Mtaa wa FFU, kata ya Muriet mkoani Arusha, Steven Jacob (35), aliyekuwa ametekwa na watu wasiojulikana, waumini wa kanisa hilo nchini wameeleza namna walivyokimbilia kanisani kuomba kwa saa kadhaa.
Waumini hao wamesema hawakuwa na namna yoyote wala hawakujua nini kingine wanaweza kufanya zaidi ya kukimbilia kanisani kumuomba Mungu.
Leo Jumapili, Mei 18, 2025, ibada kanisani hapo iliongozwa na Mchungaji Vulfrida George akisaidiana na baba wa mchungaji huyo, Jacob Gumbo ambaye pia ni mchungaji wa kanisa hilo na balozi wa nyumba 10 wa Chama cha Mapinduzi (CCM).

Mwonekano wa nje wa Kanisa la Huduma ya Kristo lililopo Mtaa wa FFU,Kata ya Muriet mkoani Arusha ambalo Mchungaji wake Steven Jacob,alitekwa juzi Mei 16,2025 kabla ya kupatikana jana huko eneo la West Kilimanjaro,wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro.Picha na Janeth Mushi
Katika ibada hiyo, waumini wa kanisa hilo, tawi la Arusha, waliungana na wenzao wa matawi mengine, ikiwemo kutoka jijini Dar es Salaam na Iringa kueleza namna walivyosali kwa saa kadhaa kufuatia tukio hilo.
Mmoja wa waumini hao kutoka Buza (Dar es Salaam) ambaye hakujitambulisha, ameeleza kuwa mioyo yao ilivuja damu, kwani walihuzunika kufuatia tukio hilo, ila walikimbilia kanisani kusali wakimuomba Mungu amrejeshe salama kiongozi wao.
“Sisi Iringa hatuna la zaidi ya kumshukuru Mungu kwa sababu ya matendo makuu ambayo kila siku anatuonyesha. Baada ya kupata hizi taarifa, hatukuwa na pa kwenda, tulienda mbele za Mungu na tunamshukuru Mungu kwani hajatuacha, tumepokea ushindi,” amesema.
Akihubiri katika ibada hiyo, Mchungaji Vulfrida amesema kuwa ibada ya leo ni kumshukuru Mungu, huku akifananisha changamoto hiyo na baadhi ya matukio yaliyowahi kutokea katika Biblia, ikiwemo la Paulo na Sila waliokuwa gerezani ambao walisali hadi milango la gereza ikafunguka.
“Juzi tulipopata hii changamoto, kwani kwa Mungu hakuna kinachoshindikana, kwa kweli nililinganisha na matendo ninayosoma kwenye Biblia, watu waliopitia mambo kama hayo nikaona wakishinda kwa jinsi walivyoingia katika maombi,” amesema Mchungaji Vulfrida.
“Nasi tukajua tunapaswa kuingia katika maombi katika hali kama ile, tulikuwa hatuna namna yoyote. Unakaa unajiuliza niende wapi, nifanye nini, lakini jibu liko kwa Mungu. Tuliingia kwenye maombi leo na sisi tuko hapa kwa ajili ya kumshukuru tu Mungu.
Jambo lililomkuta mchungaji wetu lilikuwa kubwa, lakini niliamini kwa Mungu anaweza, kama ambavyo kwenye Biblia, Shedrack, Meshaki na Abednego nao walipitia changamoto ambayo ilikuwa kubwa lakini walienda kumuona Mungu wao aliyewaokoa,” amesema.
Baba yake atia neno
Akizungumza katika ibada hiyo, Gumbo ambaye ni baba mzazi wa Steven, amesema baada ya kijana wake kutekwa na watu hao, alilazimika kuwaambia waumini waingie kanisani kwa ajili ya maombi, wakisali kwa saa nyingi.
Mchungaji Gumbo akinukuu katika kitabu kitakatifu cha Biblia kutoka Zaburi 105:15, ambayo inasema “Akisema msiwaguse masihi wangu, wala msiwadhuru nabii zangu,” amewataka vijana waliohusika na tukio hilo kutubu.
Aidha, amewaonya wanaowagusa kwa kuwaumiza na kuwatesa viongozi wa dini na kuwataka waache vitendo hivyo mara moja, akiongeza kuwa endapo kuna tatizo ni vema hekima ikatumika na kuwaita na kuzungumza nao.
“Wale vijana kama watasikia sauti yangu mahali walipo, wamuombe Mungu sana maana Zaburi 105:15, siyo maneno yangu, ni ya Mungu. Leo masihi wa Mungu wanapigwa, wanateswa. “Nawaonya wale wanaogusa watumishi wa Mungu kwa kuwapiga au kuwatesa, nawaambia neno la Mungu litakuwa juu yenu, Bwana atajua jinsi gani ya kuweza kuwashughulikia. Vijana mliofanya tukio hili msione mmefanikiwa,” amesema.

Baadhi ya waumini wa Kanisa la Huduma ya Kristo lililopo Mtaa wa FFU,Kata ya Muriet mkoani Arusha wakiwa nje ya Kanisa hilo leo Jumapili Mei 18,2025 baada ya kumalizika kwa ibada.Picha na Janeth Mushi
Gumbo ameeleza kuwa baada ya kutokea jambo hilo, akiwa anasali alitafakari na kutamani kutamka maneno ambayo yangekuwa laana kwa waliotenda kosa hilo, lakini alizuiwa na kukumbushwa kuwa waliofanya kitendo hicho akiwatamkia maneno hayo yataumiza vizazi vyao.
“Niliambiwa kumbuka wale waliofanya hivyo ni vijana kama wako, usije ukatamka hayo maneno kwa sababu utawauwa. Wanaweza kudhani kwa kipindi hiki wamefanikiwa sana, lakini vizazi vyao vitaharibikiwa.
“Sikutaka kuyatamka yale na kwa kweli. Yako mambo ambayo yanaonekana ni ya kawaida, lakini siyo kawaida. Huko zamani watu walikuwa hawaendi vitani au kufanya lolote bila kumuona nabii (muonaji), wakiambiwa hawatashinda hawaendi, kwa sababu wanajua hiyo ni sauti ya Mungu,” amesema.
Mchungaji asimulia
Akisimulia tukio hilo, Mchungaji Jacob amedai waliomteka walimpeleka hadi eneo la West Kilimanjaro lililopo Wilaya ya Siha, mkoani Kilimanjaro, ambako walichukua simu zake wakimtaka afute picha mjongeo (video) alizokuwa amepandisha kwenye mtandao wa YouTube.
“Naomba nisiongee mengi kwa sababu ni ishu za mtandao nilizo-post YouTube. Baada ya kunipiga na kuchukua baadhi ya maelezo, ambayo nafikiri nisingependa kuyaongea, nikasikia kama wananipeleka mahabusu, ila haikuwa hivyo, wakanipeleka porini West Kilimanjaro.
“Walivyotaka nifute video, kwa bahati mbaya bundle (kifurushi cha intaneti) kilikuwa kimeisha, ikabidi wafanye mpango wapate bando, wakasema wawili au mmoja abaki na mimi, halafu wengine wakatafute bando ili nifute video,” amesimulia.
Mchungaji huyo amesema watu hao walimwambia alale chini, wakamkanyagia shingoni, na mmoja wao akawaambia wenzake wanamuachaje hapo. Basi, wakamuacha wakaondoka na simu yake.