Waumini wa Kiislamu waibua mjadala adhabu ya fimbo madrasa

Dar/Mikoani. Viongozi na waumini wa dini ya Kiislamu, wameeleza wasiwasi wao kuhusu matumizi ya adhabu kali kwa watoto wanaosoma madrasa, wakisisitiza zinazotolewa lazima ziwe za mafunzo na za kumjenga mtoto kiroho na kimaadili, badala ya kumuumiza.

Kauli hiyo imetokana na mahojiano yaliyofanywa na Mwananchi kutokana na malalamiko kwenye mitandao ya kijamii kuhusu adhabu za viboko zinazotolewa na baadhi ya walimu wa madrasa.

Japo wapo waliounga mkono adhabu hiyo, walioipinga wanasema walimu wa madrasa hawana budi kuwa na weledi wa kutosha wa ualimu, ikiwamo saikolojia ya watoto ili kutoa adhabu kwa njia inayojenga na kufundisha, badala ya kuwaumiza.

Kauli ya Bakwata

Katikati ya mjadala huo unaoendelea, Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), limeeleza lengo halisi si kutoa adhabu bali ni malezi bora kwa watoto.

Katibu Mkuu wa baraza hilo, Alhaji Nuhu Mruma akizungumza na Mwananchi amesema ingawa hakuna mwongozo mahususi kuhusu adhabu, wanatarajia walimu kuwa waangalifu na kuwalea watoto kama wazazi, badala ya kutumia fimbo kama njia kuu ya kutoa adhabu.

Mruma amesisitiza mwalimu katika madrasa ni kama mzazi na ana haki ya kutoa adhabu, lakini haipaswi kumdhuru mtoto. Amesema adhabu inapaswa kutolewa kwa kuzingatia umri na mazingira ya mtoto.

Amekiri kuwa walimu wengi hawana elimu ya saikolojia inayohitajika ili kuwasaidia kuwafahamu watoto.

“Hivyo, Bakwata imeanzisha semina na kozi maalumu kwa walimu ili kuwaandaa kitaalamu,” amesema.

Amesema tangu miaka mitano iliyopita walipoanzisha kozi kwa walimu, ikiwa ni pamoja na masomo ya mtandao kupitia Bakwata Online Academy, zaidi ya walimu 300 wamepata mafunzo.

Mruma amesema Bakwata imeanzisha kanzidata ya walimu wa madrasa ikilenga kuwafuatilia kwa urahisi na kuchukua hatua haraka pindi yanapotokea matatizo.

Amewashauri wazazi kuhakikisha wanawafahamu walimu wa watoto wao kabla ya kuwapeleka madrasa ili kuepuka matatizo ya adhabu kali.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Walimu wa Quran Tanzania, Sheikh Alhad Musa Salum, ameungana na msimamo wa  Bakwata na kuongeza kuwa, adhabu ya fimbo inaruhusiwa kidini kama itatolewa kwa njia ya kujenga na siyo kumuumiza mtoto.

Amesisitiza suala la kumchapa mtoto halina dhambi, lakini linapaswa kufanyika kwa kuzingatia umri na hali ya mtoto.

Mwalimu wa madrasa, Ustadhi Ghadaf Kombo, amesema kwao fimbo si kipaumbele, bali amekuwa akihakikisha wanafunzi wanajitahidi kwa kuwapa zawadi wale wanaofanya vizuri na kutumia fimbo mara chache.

Kaimu Katibu Mtendaji Ofisi ya Mufti Zanzibar, Khamis Gharib Khamis amesema licha ya adhabu kuruhusiwa lakini zinatakiwa zitolewe kulingana na umri wa mtoto na kwa kiasi.

“Ofisi ya Mufti inawasihi walimu wote wa madrasa kuwa waangalifu wakati wa kuwaadabisha wanafunzi na kujiepusha na adhabu za kuumiza mwili ili kuwajenga vyema wanafunzi katika kuisoma elimu ya dini,” amesema.

Mwalimu wa madrasa katika msikiti wa Tawfiq uliopo Soweto, jijini Mbeya, Sheikh Hassan Mbarazi amesema wanaotoa adhabu kali kwa wanafunzi wa elimu ya dini wachukuliwe hatua na mamlaka za dini.

Amesema elimu ya dini ni mahususi kwa ajili ya malezi kwa watoto, hivyo wanaofanya vitendo hivyo baadhi yao ni ama hawana mafunzo rasmi ya ualimu au wana msongo wa mawazo.

“Wanaofanya hivyo washughulikiwe na chombo cha dini (Bakwata), mtoto anapokosea anaelekezwa, madarsa zipo tofauti. Malezi ya madrasa ni ya kiroho ili aweze kunyooka.

“Iwapo mtoto atakosea kuna adhabu za kutolewa kulingana na umri wake, lakini kuna namna ya kumuadhibu. Unamkuta mwalimu mwingine ana hasira, katika madrasa yetu Tawfiq mwalimu akifanya hivyo tunaweza kumsimamisha,” amesema.

Imam wa Msikiti wa Nunge jijini Dodoma, Abdallah Sadiki amesema adhabu za viboko katika madrasa zipo, lakini siyo kwa kiwango kikubwa.

Ameeleza kwa kiasi kikubwa adhabu inayotumiwa na wengi ni vitisho kwa watoto.

Sadiki amesema adhabu yoyote inapopita kiwango huwa mbaya, kwani inahama kutoka kwenye mafundisho na kuwa sehemu ya mipango ya kudhuru mwili.

“Unamtisha mtoto kiasi halafu mambo yanakuwa mazuri na nidhamu inakuwepo, kama ni viboko basi viwe vya kiasi,” anasema.

Sheikh wa Mkoa wa Dodoma, Alhaj Mustafa Shaban aliyewahi kufundisha madrasa katika shule za Hijra na Jamhuri amesema kuna haja ya walimu kujifunza somo la saikolojia.

“Saikolojia ni somo muhimu, watu wengi wanakurupuka kwenda kufundisha watoto huku wakikosa maadili. Ufike wakati tuwafunze somo hilo kwanza kabla ya kuwakabidhi watoto,” amesema.

Kauli za wazazi

Yusra Kassim, mkazi wa Mabibo, Dar es Salaam anasema watoto huwa wanachapwa wakiwa madrasa hivyo amelazimika kuwatafutia wa kwake mwalimu wa kuwafundisha nyumbani.

Yusra anasema tatizo analoliona ni kuwa walimu wameshindwa kutofautisha kwamba kuna watoto wanaoelewa haraka na wengine wana uelewa mdogo.

“Mfano, mtoto wangu wa kiume alikuwa anachapwa sana kuliko wa kike, lakini baada ya kumwelewesha mwalimu niliyempata hapa nyumbani alijua namna ya kwenda naye na niliona mabadiliko,” anasema.

Neema Msuya, mkazi wa Ukonga, Dar es Salaam, anasema mtoto wake alipenda kwenda madrasa lakini baadaye alikataa kutokana na kuchapwa.

Imeandikwa na Nasra Abdallah (Dar), Rajabu Athumani (Tanga), Jesse Mikofu na Zuleikha Fatawi (Zanzibar), Saddam Sadick (Mbeya), Habel Chidawali (Dodoma) na Saad Amir (Mwanza)