Watumishi wengine 26 wa LBL wakamatwa Dar

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, limewakamata watuhumiwa 26 kwa tuhuma za kujihusisha na biashara haramu ya upatu mtandaoni, bila vibali vya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Watuhumiwa hao waliokamatwa kwa siku tofauti, ni sehemu ya wafanyakazi wa Kampuni ya Leo Burnett London (LBL), akiwamo mkurugenzi wao, Najim Houmud.

Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi, watuhumiwa hao walikamatwa kuanzia Februari 18 hadi 22, 2025.

Awali, jeshi hilo, lilitangaza kuwatia nguvuni watu 12 kutoka mikoa ya Morogoro na Mbeya kwa tuhuma hizo hizo, hivyo hadi sasa jumla ya waliokamatwa inafikia 38.

Kampuni hiyo inadaiwa kuwachangisha wanachama wake Sh50,000 ada ya kiingilio ili wapate faida ya kila siku kwa kusambaza vipande vya video wanazotumiwa.

Taarifa ya kukamatwa kwa watuhumiwa hao, imetokewa Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Faustine Mafwele, jana Jumatatu, Februari 24, 2025.

Baadhi ya waliokamatwa ni Hatibu Kudura (25) mkazi wa Kinondoni, Fatum Hamisi (26) mkazi Kigamboni na Athumani Sadik (29) mkazi wa Mabibo.

Maeneo waliyokamatiwa kwa mujibu wa jeshi hilo ni Mbagala, Gongolamboto, Tabata, Mbezi Magufuli, Ubungo Riverside na Mabibo.

Hatua ya kukamatwa kwao, ni matokeo ya uchunguzi wa jeshi hilo na BoT, uliobaini kampuni hiyo haina uongozi maalumu.

“Vilevile ufanyaji kazi wake unahusisha kuwatoza wananchi kuanzia Sh50,000 na kuendelea ili uwe mwanachama, pia huchangisha fedha kwa kuwadanganya wananchi kuwa watapata faida kubwa kwa muda mfupi bila ya wanachama kuhusishwa kwa namna yoyote katika shughuli za uendeshaji wa kampuni hiyo,” inaeleza taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa jeshi hilo, baada ya upelelezi kukamilika watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.

“Jeshi la Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam linatoa wito kwa wananchi wote kuacha kujihusisha na biashara za upatu mitandaoni bila kujiridhisha kwanza kwa kuwa baadhi ya biashara hizo hazina leseni wala vibali kutoka mamlaka za kisheria zinazohusika, hivyo kuhatarisha usalama pesa zao,” inaeleza.