Unguja. Wafanyakazi wa taasisi mbalimbali za Serikali wametakiwa kufuata sheria za utumishi wa kazi kwa kutunza nidhamu, weledi, uadilifu na uwajibikaji ili kutekeleza majukumu yao kwa wakati.
Kauli hiyo imetolewa leo, Machi 27, 2025, na Mkurugenzi Idara ya Utumishi na Uendeshaji wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Rashid Makame Hamdu, katika mafunzo ya sheria za kazi kwa watumishi.
“Iwapo wafanyakazi watafuata sheria za utumishi wa kazi kwa kutunza nidhamu, weledi, uadilifu na uwajibikaji, kutasaidia kujiamini katika utekelezaji wa majukumu yao na kufanyakazi kwa ufanisi,” amesema Rashid.
Pia, amesema kila mtumishi anapaswa kutekeleza majukumu yake ya kiutendaji ili kufikia lengo lililokusudiwa.

Mkurugenzi huyo amesema ni vyema wafanyakazi wote kuzingatia misingi na usalama wa afya zao, kujua athari zinazoweza kutokea wakati wanapokuwa kazini kutokana na mazingira yaliyopo ndani ya ofisi zao.
Akiwasilisha mada ya sheria kwenye mafunzo hayo, Yahya Saleh Salim amesema asiyetii sheria pamoja na miongozo ya kiutumishi atakuwa amevunja maadili na miiko ya kazi, hivyo watumishi wote wafanye kazi chini ya sheria zilizopo.
Ameeleza kuwa watumishi wa Serikali hawapaswi kutoa taarifa za Serikali au siri za Serikali kwa watu wasiohusika, kwani kufanya hivyo ni kosa la kimaadili.
Hata hivyo, amewataka wafanyakazi hao kudumisha maadili mema na kufuata masharti yaliyowekwa katika kanuni, ikiwemo kufanyakazi kwa wakati.
Naye Ofisa Masilahi kutoka Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Mustafa Khamis Simai, amesema ni wajibu wa kila mtumishi wa umma kufanyiwa upimaji na tathmini katika utekelezaji wa kazi zake za kila siku ili kupatikana haki zake.
Amesema Serikali haitofanikiwa bila ya wafanyakazi kutekeleza majukumu yao kiufanisi na kujiepusha na uzembe utakaosababisha kuishushia hadhi ofisi na mtumishi wake.
Vilevile, amewaasa wafanyakazi hao kutofanya vitendo vitakavyowavunjia heshima, ikiwemo kujiingiza kwenye madeni ambayo mtumishi atashindwa kuyalipa.