Dar es Salaam. Waajiri wa sekta binafsi nchini Tanzania wameshauriwa kuruhusu watumishi wao katika Mkoa wa Dar es Salaam kufanyia kazi nyumbani au kuweka utaratibu ambao hautasababisha changamoto ya usafiri kutokana na kufungwa barabara tisa kwa muda.
Barabara hizo zitafungwa kwa muda kufuatia mkutano wa wakuu wa nchi za Afrika kuhusu nishati utakaowakutanisha zaidi ya marais 25, viongozi mbalimbali katika mkutano huo utakaoanza kesho Jumatatu Januari 27 hadi na 28, 2025 jijini Dar es Salaam.
Wakati hilo likishauriwa, watumishi umma katika Mkoa wa Dar es Salaam wameelekezwa kufanyia kazi nyumbani isipokuwa wale ambao mazingira yao ya kazi yanawataka kuwepo katika vituo vya kazi.
Wito huo umetolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Dk Moses Kusiluka kupitia taarifa yake kwa umma aliyotolewa leo Jumapili Januari 26, 2025 ikiwa ni siku moja kabla ya kuanza kwa mkutano huo utakaofanyikia ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC).

Dk Kusiluka amesema jumla ya washiriki 2,600 wa ndani na nje ya Tanzania wamejisajili kwa ajili ya mkutano huo jambo ambalo litafanya baadhi ya barabara muhimu za jiji la Dar es Salaam kufungwa kama ilivyotangazwa na Jeshi la Polisi.
“Hivyo, ili kuepuka usumbufu ambao unaweza kusababishwa na kufungwa kwa barabara hizo, Serikali inaelekeza tarehe 27 na 28 Januari, 2025 watumishi wa umma katika Mkoa wa Dar es Salaam wafanyie kazi nyumbani isipokuwa wale ambao mazingira yao ya kazi yanawataka kuwepo katika vituo vya kazi,” amesema.
Miongoni mwa wanaotakiwa kuwa kazini ni watumishi wa vyombo vya ulinzi na usalama, sekta ya afya na sekta ya usafiri na usafirishaji.
“Waajiri katika sekta binafsi wanashauriwa kuruhusu watumishi wao katika Mkoa wa Dar es Salaam kufanyia kazi nyumbani au kuweka utaratibu ambao hautasababisha changamoto ya usafiri kutokana na kufungwa kwa barabara hizo,” amesema.
Katibu mkuu huyo kiongozi amesema: “Vilevile, Benki hazitafungwa na biashara katika Soko la Kariakoo zitaendelea kufanyika. Hoteli na migahawa nayo haitafungwa.”
Tanzania imepata fursa ya kuwa mwenyeji wa mkutano wa wakuu wa nchi za Afrika kuhusu nishati (Africa Energy Summit) utakaofanyika jijini Dar es Salaam ambao umeandaliwa kwa pamoja baina ya Serikali ya Tanzania, Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo ya Afrika.
Mkutano huu utajumuisha marais wa nchi za Afrika 25 wakiongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, wawakilishi wa wakuu wa nchi na Serikali za Afrika 21.
Wengine ni wakuu wa Taasisi za kimataifa sita akiwemo rais wa Benki ya Dunia, rais wa benki ya Afrika na Rais wa Taasisi ya Rockefeller na washirika wa maendeleo watano watashiriki mkutano huo.
Taarifa ya Polisi iliyotolewa jana Jumamosi Januari 25, 2025 na Kamanda wa Kanda Maalumu ya Polisi Dar es Salaam, Jumanne Muliro, imesema kutokana na ugeni huo, barabara tisa zitafungwa kuanzia leo Jumapili.
Barabara zitakazofungwa
Taarifa ya Polisi iliyotolewa jana Jumamosi Januari 25, 2025 na Kamanda Kanda Maalumu ya Polisi Dar es Salaam, Jumanne Muliro imesema kutokana na ugeni huo barabara tisa zitafungwa kuanzia siku ya taarifa hiyo iliyotolewa.
Amezitaja barabara zitakazofungwa kuwa ni Nyerere kutokea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kwenda katikati ya jiji.
Nyingine ni Barabara ya Sokoine, Kivukoni na Lithuli kuanzia taa za Gerezani kwenda Hoteli ya Johari Rotana, Hyatt Regency hadi Ikulu.
Pia ipo Barabara ya Ohio kutokea Kivukoni kwenda Hoteli ya Serena na ile ya Ghana kutokea Barabara ya Ohio kwenda Hoteli ya Onomo
Vilevile Barabara ya Bibi Titi kutokea makutano ya Barabara za Ohio na Ally Hassan Mwinyi kwenda Hoteli ya Crowne na Barabara ya Azikiwe kwenda Hoteli ya Four Points, Hoteli ya Golden Tulip City Center na Hoteli ya Holiday Inn.
Pia, ipo Barabara ya Morogoro kutokea Sokoine kwenda Hoteli ya Tiffany No. 1 na ile ya Makunganya kutokea Azikiwe kwenda Hoteli ya Tiffany No. 2.
Aidha Barabara ya Garden kutokea Barabara ya Lithuli kwenda Hoteli ya Southern Sun pamoja na Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa JNICC nayo itafungwa kutokana na ugeni huo.