
Dar es Salaam. Ni mtikisiko! Ndivyo unavyoweza kusema baada ya sintofahamu kutawala miongoni mwa watumishi waliokuwa chini ya miradi ya ufadhili wa Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID), wengi wakihofu kukosa mishahara na ajira zao.
Sintofahamu hiyo imekuja baada ya Januari 20, 2025 Rais wa Marekani, Donald Trump kutoa tamko la kusitisha kwa siku 90 misaada ya maendeleo ya nje, kupisha tathimini ya ufanisi na uwiano na sera yake ya kigeni, hali iliyowalazimu wasimamizi wa ufadhili nchini kusitisha miradi.
Miongoni mwao wamesimamishwa kazi ili kutekeleza amri ya kiutendaji iliyosainiwa na kiongozi huyo.
Kwa mujibu wa Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Mugisha Nkoronko maelekezo hayo yameitikisa sekta ya afya kwa kuwa baadhi ya wataalamu walio kwenye vituo vya afya mijini na vijijini nchini, wanategemea mishahara kutoka mashirika yanayopata ufadhili kutoka Marekani.
Dk Nkoronko amesema watumishi wanaofanya kazi moja kwa moja kwenye mashirika hayo na asasi za kiraia, asilimia kubwa wapo katika sekta ya afya, walioajiriwa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya vya umma ambao mishahara yao inatoka katika shirika hilo.
Amewataja kuwa ni wale wanaoibua wagonjwa kwenye jamii na wahamasishaji wa kupima Virusi vya Ukimwi (VVU).
“Kuna madaktari, wauguzi wameajiriwa vituo kadhaa, ustawi wa jamii, wataalamu wa maabara, maofisa miradi wanaofanya tathmini ya miradi, wahasibu, wanaoshughulika na ugavi, wafanyakazi kada ya kati ya tiba, matabibu na wengine wengi,” amesema.
Amesema karibu kila kada kwenye afya ilipata nafasi ya kufanya kazi kwenye miradi mbalimbali inayohusishwa na USAID au PEPFAR.
Hata hivyo amesema wasimamizi wa mashirika hayo wamechukua hatua za haraka kuwasimamisha kazi watumishi kwa kuwa tangazo lilikuwa ni ukaguzi wa miezi mitatu.
“Hili jambo linatakiwa kutazamwa upya, huduma zitaathirika watumishi watapungua, wengine wana wasiwasi, inawezekana wakapunguzwa au wasipunguzwe na wengine wakakosa ajira. Mamlaka zinazohusika zitumie utashi kushughulikia jambo hili ili kuziba zile nafasi kuzuia wafanyakazi waliopo kufanyakazi zaidi,” amesema Nkoronko.
Mishahara yasitishwa
Mmoja wa watumishi aliyeajiriwa na Shirika la MDH amesema hali imeanza kwenda vibaya baada ya wiki iliyopita kutangaziwa suala la mishahara wasubiri kwanza.
“Trump ametutenda aisee! Wiki iliyopita tulitangaziwa kuwa tuanze kufanyia kazi nyumbani, wakati suala la mishahara ya Januari tunasubiri kwanza kuona wanafanya nini,” amesema mtumishi huyo aliyeomba hifadhi ya jina lake.
Amesema tayari hali hiyo imeanza kuwasababishia msongo wa mawazo ikizingatiwa wana familia, wanategemewa, kukaa nyumbani si dalili njema na hilo linaweza kuathiri hata ufanisi wa huduma serikalini.
“Mshahara unatoka MDH, ukienda hospitali mbalimbali za Dar es Salaam kuna watumishi wa MDH, sasa wakikaa kando majukumu yao wanafanya kina nani? Au Serikali itawalipa, yaani ni mvurugano tu.
“Kuna mwenzangu yeye ameambiwa bosi wake huko anakofanya wanaangalia utaratibu wawe wanamlipa hata posho wakati anasubiri MDH wafanye jambo, kwa sababu wanaona kabisa hawatoweza. Na watumishi wa MDH wapo nchi nzima.”
Alipotafutwa kuulizwa suala hilo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la MDH, Dk David Sando amesema hakuna aliyesitishiwa mshahara bali wapo walioelekezwa wasiripoti kwenye vituo vyao vya kazi.
“Tumewapa maelekezo mpaka tutakapowaambia, kutokana na maelekezo yale ya mfuko wa Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa kukabiliana na Ukimwi (PEPFAR) ambao Trump amezuia.
“Wote walio chini ya ule mfuko. Mishahara wameshapata wa mwezi huu na ule wa mwezi ujao pia watapata,” amesema.
Hata hivyo, Dk Sando amesema leo wameshapatiwa maelekezo mapya kupitia barua ya kurudi, kwa hiyo kesho Jumatatu wote wataambiwa warudi kuripoti kwenye vituo vyao vya kazi.
Miongoni mwa mashirika yanayoajiri watumishi wa kada ya afya ni Taasisi ya Benjamin Mkapa ambayo imetoa ajira zaidi ya 13,000.
Alipotafutwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Benjamin Mkapa, Dk Ellen Mkondya-Senkoro kuhusu sakata hilo, amesema: “Nitazungumza kesho, kwa maana habari inaweza kubadilika kesho.”
Kusimamishwa kazi
Baadhi ya watumishi wa kada ya afya waliozungumza na Mwananchi leo Jumapili, Februari 2, 2025, wamesema walisimamishwa kazi tangu Januari 24, huku wengine wakisema miradi waliyokuwa wakiitekeleza imesimama.
“Tumesimamishwa kazi na miradi yote imesimama. Kuna walioambiwa wataendelea kupokea mishahara na hawa ni wale waliokuwa kwenye mashirika yanayosimamia miradi, lakini wale waliokuwa wanasubiri mishahara ya miradi wamesitishiwa kabisa kazi, wameambiwa wabaki nyumbani,” amesema mmoja wa watumishi walionufaika na miradi hiyo ambaye hakutaka kutajwa jina.
Mtumishi mwingine kutoka katika shirika kubwa amesema, “sisi tunafanyia kazi nyumbani. Lakini miradi yote imesimama na mshahara tulipata kama kawaida.”
Hata hivyo, miongoni mwa watumishi wa ngazi za chini waliozungumza na gazeti hili, wamesema wamekuwa wakisumbuliwa na walengwa waliokuwa wakipatiwa ushauri na dawa hasa wanaokijinga na VVU kupitia dawa kinga za Prep.
“Unakuta kuna waliotaka kupata marudio ya Prep labda Januari 28 na hawajapata huduma mpaka muda huu, hatuoni italeta madhara kwa ukosefu wa dawa? Lakini tuliambiwa huduma za mradi zimesimama wateja wanapiga simu mpaka unahisi mtu atapata maambukizi kwa kukosa kinga,” amesema mmoja wa waraghabishi aliyeko mkoani Mwanza.
Miradi ya USAID
Ushirikiano wa Marekani na Tanzania umedumu kwa zaidi ya miongo sita. Mpaka mwaka 2025, orodha ya miradi ya USAID ambayo imekuwa ikitekelezwa nchini ni pamoja na kilimo na upatikanaji wa chakula, demokrasia, haki za binadamu na utawala bora, ukuaji wa uchumi na biashara, elimu, mazingira, jinsia na vijana pamoja na afya.
Kwa mwaka 2023 pekee, USAID ilitoa zaidi ya Dola 400 milioni za Marekani kama ruzuku ili kuimarisha biashara, kukuza ajira na kuchochea maendeleo nchini.
Hata hivyo, baadhi ya wafanyakazi waliopo katika mashirika yanayofadhiliwa na USAID tayari wameanza kuwa na wasiwasi wa kupoteza vibarua vyao.