Watumiaji wa sponji za kuoshea vyombo kaeni chonjo

Dar es Salaam. Matokeo ya utafiti uliofanywa na wataalamu wa microbiolojia duniani, umebaini sponji za kuoshea vyombo vya chakula, zinabeba bakteria wanaoweza kusababisha madhara.

Utafiti huo uliofanywa na wataalamu kwa nyakati tofauti na kuchapishwa na BBC, umebaini sponji zina mazingira mazuri kwa bakteria kustawi, ikiwa ni pamoja na kuzaliana ingawa kwa mtu mwenye afya njema, bakteria hao si hatari kwake.

Imeelezwa bakteria wana uwezo wa kukaa maeneo mbalimbali ikiwemo kwenye baridi kali, lakini kama wangechagua makazi yao wanayopenda na bora, basi kifaa hicho kingekuwa chaguo lao la kwanza.

Sponji ambayo ndiyo kifaa kinachotumiwa kusafisha vyombo kama sahani, sufuria na glasi, inaweza kuwa na maisha ya mamilioni ya vijidudu. Aghalabu, sponji ina unyevunyevu huku ikijaa mabaki ya chakula yanayowapa bakteria lishe wanayohitaji.

Mwaka 2017, Markus Egert, mtaalamu wa Microbiolojia kutoka Chuo Kikuu cha Furtwangen nchini Ujerumani, alichapisha utafiti kuhusu mikrobiomu ya bakteria waliopo ndani ya sponji.

Katika utafiti wake, Egert aligundua sponji zilikuwa na aina 362 za bakteria. Katika baadhi ya maeneo, msongamano wa bakteria ulifikia hadi bilioni 54.

“Hiki ni kiwango kikubwa sana, ni sawa na idadi ya bakteria inayopatikana katika kinyesi cha binadamu,” anasema Egert.

Utafiti wa Egert unaungwa mkono na utafiti uliofanywa mwaka 2022 na Lingchong You, mtaalamu wa biolojia ya sintetiki kutoka Chuo Kikuu cha Duke, ambapo alionesha jinsi mazingira ya sponji yanavyosaidia ukuaji wa vijidudu hao.

Timu yake iligundua kuwa sponji zilizo na matundu ya ukubwa tofauti, ndizo zilizosaidia bakteria kukua kwa kasi zaidi.

“Hili lina mantiki kwa sababu bakteria wana tabia tofauti kuna wale wanaopenda kuwa peke yao, na kuna wale wanaohitaji kuwa na wenzao. Ndani ya sponji kuna nafasi nyingi zinazowafaa wote,” anasema Egert.

Daktari Isaya Mhando akizungumza na Mwananchi, amesema mabaki ya vyakula ndio yanayokuwa chakula cha bakteria hivyo inafanya bakteria hao kuishi kwa raha zao.

Hata hivyo, utaifit umesema, bakteria wapo kila mahali kama kwenye ngozi, udongo na hata angani na si wote ni hatari.

 “Kwa kawaida, kwa mtu mwenye afya njema, bakteria waliopo kwenye sponji si hatari,” amesema.

Watafiti wamesema mbinu maalumu za kusafisha kama vile kupasha sponji moto kwenye microwave au kuisuuza kwa maji ya moto na sabuni hazikusaidia sana. Ingawa baadhi ya bakteria waliuawa, hatua hizi ziliwaruhusu aina nyingine sugu kustawi zaidi.

Mwaka 2017, Jennifer Quinlan, Profesa wa usalama wa chakula katika Chuo Kikuu cha Prairie View A&M, Marekani, na wenzake walikusanya sponji kutoka nyumba 100 jijini Philadelphia.

Waligundua kuwa ni asilimia moja hadi mbili pekee ya sponji hizo zilikuwa na bakteria wanaohusiana na sumu ya chakula kwa binadamu, na hata hivyo, idadi yao ilikuwa ndogo.

Matokeo haya yalithibitishwa na utafiti wa mwaka 2022 uliofanywa na Solveig Langsrud, mwanasayansi katika taasisi ya utafiti wa chakula ya Norway, Nofima, ambapo alilinganisha bakteria waliopo kwenye sponji za kusafishia vyombo na brashi.

Aligundua kuwa vyombo vyote viwili vilikuwa na seti ya bakteria wasio na madhara, ikiwa ni pamoja na Acinetobacter, Chryseobacterium, Enhydrobacter, Enterobacteriaceae, na Pseudomonas. Hata hivyo, brashi zilikuwa na idadi ndogo zaidi ya bakteria kwa ujumla.

Bakteria hawa wenye uwezekano wa kusababisha magonjwa wanaweza pia kuhamia kutoka kwenye sponji hadi kwenye sahani, vyombo au sehemu za jikoni.

Kwa hivyo, ingawa bakteria wengi wanaostawi kwenye sponji si hatari, iwapo bakteria wenye madhara kama Salmonella wataingia humo, basi watazaliana.

Katika utafiti wa Langsrud, watafiti walipopachika bakteria wa Salmonella kwenye sponji za jikoni, walistawi kwa wingi. Lakini walipowaweka kwenye brashi, walikufa. Sababu moja inaweza kuwa kwamba brashi hukauka haraka, hivyo huua bakteria wa Salmonella, ilhali sponji hubaki na unyevunyevu kwa muda mrefu ikiwa inatumika kila siku.

Kwakuwa sponji ya kuoshea vyombo ina mazingira mazuri kwa bakteria kukua kwa sababu ya unyevunyevu, mabaki ya chakula, na joto. Bakteria hawa wanaweza kuwa na madhara ikiwemo kusababisha maambukizi ya tumbo ikiwemo tumbo kuuma kuhara na kutapika.

Ufanye nini?

Unapaswa kuosha sponji mara kwa mara kwa maji moto na sabuni.

 Chemsha kwa sekunde 60 ili kuua bakteria.

 Badilisha sponji mara kwa mara (angalau kila wiki moja au mbili).

Mbadala wa sponji

Wataalamu wanashauri kuwa tunapaswa kuibadilisha sponji kila wiki. Hata hivyo, kuna mbinu za kuifanya idumu kwa muda mrefu. Aidha, wanashauri kuosha vyombo kwa kutumia brashi kwa sababu hukauka haraka na huhifadhi vijidudu vichache

“Kuna njia ya kupasha moto kwenye microwave kwa dakika moja hadi mvuke uanze kutoka. Hii itaua vijidudu vingi vya magonjwa,” anasema Quinlan huku ikibainika kufanya hivyo kunaweza kupunguza idadi ya bakteria kwa ufanisi zaidi kuliko kuiloweka kwenye maji yenye dawa ya kuua viini.

Rahma Ramadhan kutoka Tabata anasema sponji ameizoea na hakuwa anafahamu kama ina bakteria ingawa kwanzia sasa ataanza kutumia brashi.