
Morogoro. Katika msako maalumu ulioendeshwa na Jeshi la Polisi mkoani wa Morogoro katika kukabiliana na wimbi la matapeli wa mitandaoni, vijana 399 wameokolewa kutoka mikononi mwa matapeli huku watu 19 wanaojifanya viongozi wa makampuni mbalimbali wameshikiliwa kwa tuhuma za kuhusika na utapeli huo.
Katika taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoa Morogoro, Alex Mkama aliyoitoa leo Aprili 2, 2025 imeeleza kuwa katika msako maalumu wa kukabiliana na wimbi la matapeli hao wa mitandaoni wamefanikiwa kuwakamata watu hao Kwa tuhuma za kuhusika na utapeli huo.
Kamanda Mkama amesema matapeli hao wamekuwa wakiwarubuni vijana kwamba wanawafundisha namna ya kuwa mabilionea wa baadaye kutumia majina ya makampuni ambayo yanachunguzwa kuhusu uhalali wake.
“Vijana hao wanashawishiwa kufika eneo watakaloelekezwa (nyumba kubwa zenye uzio) ambapo hulipa ada ya mafunzo kati ya 600,000 hadi 1,00,000. wakishapokelewa huanza kulazimishwa kuwashawishi wenzao ambapo huwavuta kwa maneno mazuri na kusafiri kutoka walipo hadi mkoani Morogoro katika kambi walipo wao kujumuika nao kwenye mafunzo hayo ya utapeli,” amesema Kamanda Mkama.
Amesema vijana wengi wanatoka mkoani Arusha, Manyara, Tanga, Kilimanjaro, Mwanza na Iringa na kwamba wakiwa kambini huanza kuwalazimisha wazazi wao wawatumie fedha kwa ajili ya kuendelea na mafunzo zaidi, huku wakiaminishwa kuwa watakapohitimu watapatiwa ajira kupitia mitandao.
“Kuna mama mmoja yeye mtoto wake anamtishia kwamba yupo tayari kuuza figo kama hayupo tayari kumtumia fedha za kusafiri kwenda huko ng’ambo (nje ya nchi) kwa ajili ya kuwa bilionea, lakini mwisho wa siku wanaachwa solemba wanakuja kwenye vituo vya Polisi kutoa taarifa kupata msaada wa kurejeshwa kwao,” amesema Kamanda Mkama.
Aidha Polisi wamesisitiza kuwa Serikali ina utaratibu rasmi wa kutoa mafunzo ya ujasiriamali kupitia vyuo vinavyotambulika, hivyo ni muhimu kwa wananchi kuwa makini ili kuepuka kudanganywa na watu wasioweza kufuatiliwa kwa haraka.
Rosemary Mtalo, Diwani Viti maalumu Kata ya Malula, Halmashauri ya Wilaya ya Arumeru Mkoa wa Arusha, mmoja kati ya ambao kijana wake ametapeliwa na matapeli hao akiwa Kibaha mkoani Pwani katika mafunzo kwa vitendo (Field) ya Hoteli Menejiment.
“Akiwa Kibaha amekutana na dada ambaye alimuomba amuandalie Pizza, baada ya kumpelekea akampongeza kwa kuandaa vizuri kisha akamuomba mawasiliano yake akimuahidi atamtafutia kazi kisha akampa Sh7,000 kama zawadi, baada ya siku tatu akampigia simu aje Morogoro kuna kazi lakini anatakiwa aje na kiasi cha fedha Sh150,000, kwaajili ya usaili, tukampa fedha hiyo pamoja na nauli,” amesema Mtalo akiwa Kituo cha Polisi mkoani Morogoro.
Mtalo, ameongezea kuwa “Baada ya siku tatu akatupa taarifa kuwa watu 6 kati ya 30 wamepita kwenye usali na kijana wetu ameshika nafasi ya kwanza hivyo anatakiwa alipe kiasi cha fedha Sh5.8 milioni kwenda nje ya nchi (Dubai) kufanya kazi ambayo kwa mwezi atalipwa Sh2 milioni,” amesema Mtalo akiwa Kituo cha Polisi mkoani Morogoro.
Ameshukuru ushirikiano wa Jeshi la Polisi kufanikisha kuwaokoa vijana hao, huku akisisitiza wazazi na walezi kuwa makini na watoto wao pindi wanapowapa taarifa za namna hiyo ili wasiweze kuingizwa kwenye mtego huo wa kurubuniwa.