
Tanga. Watu watatu wamekutwa wamefariki dunia kwa kuchomwa moto na watu wasiojulikana eneo la msitu wa Hifadhi ya Korogwe Fuel, uliopo Kijiji cha Sindeni wilayani Handeni mkoani Tanga.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 24, 2024 kuhusu tukio hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Almachius Mchunguzi amesema tukio hilo limetokea jana Septemba 23, saa tatu usiku.
Amesema Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi kuwatafuta wahusika.
Kamanda amesema walipokea taarifa ndani ya msitu huo kuna gari ndogo inaungua moto na pembeni yake kuna watu wawili wanaungua.
Kamanda amesema askari polisi walifika eneo hilo na kukuta kuna gari ndogo linaungua moto na pembeni yake kukiwa na watu wawill wameungua kwa moto na kufariki dunia wakiwa pembeni ya gari hilo.
Mchunguzi amesema baada ya uchunguzi wa awali ilibainika miili iliyokuwa nje ya gari ni ya jinsia ya kike na ndani ya gari kiti cha nyuma ulionekana mwili mwingine ambao umeungua moto hadi kupoteza sura na haijabainika ni wa jinsia gani.
Amesema Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi kwa kushirikisha na vyombo vingine vya uchunguzi kubaini walioteketea kwa moto ni kina nani, nini kiliwatokea kabla ya umauti na waliofanya tukio hilo ni watu gani ili wakamatwe na kufikishwa mahakamani.
Amesema miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Handeni, kwa ajili ya uchunguzi.
Kamanda Mchunguzi ametoa rai kwa wananchi kushirikiana na Polisi kwa kutoa taarifa zitakazosaidia kukamilisha uchunguzi wa tukio hilo.
Msitu wa Korogwe Fuel unamilikiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Wilaya ya Handeni.