Watu wanne wameripotiwa kuuawa katika shambulio la kombora la Urusi kwenye jengo la hoteli katika Mji wa Kryvyi Rih wengine 31 wakijeruhiwa vibaya kulingana na taarifa ya gavana wa eneo husika.
Imechapishwa:
Dakika 1
Matangazo ya kibiashara
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy ameandika kuhusu shambulio hilo kwenye hoteli akisema wafanyikazi wa kujitolea kutoka Ukraine, Marekani na Uingereza wamenusurika kwenye tukio hilo.
Vilevile amechapisha video kwenye mitandao ya kijamii ikiwaonyesha wafanyikazi wa huduma za dharura wakiwaondoa watu kutoka kwenye hoteli hiyo iliyoharibiwa vibaya.
Reuters imethibitisha kutokea kwa shambulio hilo kwenye eneo hilo japokuwa haikuweza kueleza ni lini video iliyochapishwa na rais Zelensky ilirekodiwa.
Naye gavana wa eneo hilo Serhiy Lysak amethibitisha kwamba watu 14 kati ya 31 ambao walijeruhiwa kwenye shambulio hilo wako katika hali mbaya.
Idara ya majanga ya dharura hadi tukichapisha taarifa hii ilikuwa ikiendelea na shughuli za uokozi.
Jeshi la Ukraine nalo limesema wanajeshi wa Urusi walirusha makombora mawili pamoja na ndege 112 zisizo na rubani usiku wa kuamkia leo.
Kryvyi Rih, eneo anakotoka rais Volodymyr Zelenskiy, limekuwa likilenga na mashambulio ya Urusi tangu ilipoanza uvamizi kamili miaka mitatu iliyopita.