Takriban watu wanne, wakiwemo raia wawili, wameuawa kwa kupigwa risasi katika makazi ya mkuu wa zamani wa Shirika la Ujasusi la Sudani Kusini Jenerali Akol Koor Kuc katika mji mkuu wa Juba, Sudan Kusini.
Msemaji wa Jeshi Meja Jenerali Lul Ruai Koang amewathibitishia waandishi wa habari kwamba mwanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Juba aliuawa kwa kupigwa risasi Alhamisi kufuatia kutoelewana kati ya vikosi vilivyowekwa katika makazi ya Kuc na wale waliofika kumkamata na kumpeleka kwenye nyumba yake nyingine huko Jebel.
Koang amesema Koor Kuc atapewa ulinzi wa ziada na jeshi huko Jebel, ili kuwazuia wanaoweza kuchukua fursa za kumdhuru afisa huyo mkuu wa zamani wa shirika la ujasusi.
Koang amewataka wakazi kuwa watulivu, akihakikisha hakutakuwa na ufyatuaji risasi tena.
Rais Salva Kiir alimfukuza kazi Kuc mwezi Oktoba na mkuu huyo wa kijasusi ameripotiwa kuwa katika kizuizi cha nyumbani.

Kiir alimteua Kuc kuwa gavana wa jimbo alikozaliwa la Warrup, ambako ukosefu wa usalama umekithiri lakini alifutwa kazi kabla ya kuchukua wadhifa huo. Hakuna sababu iliyotolewa ya Kuc kufukuzwa kazi.
Kuc alihudumu kama mkuu wa shirika la ujasusi tangu nchi hiyo ilipopata uhuru kutoka Sudan mwaka 2011.
Taifa hilo changa zaidi duniani limekumbwa na mzozo wa miaka mingi na kusababisha watu kuhama makazi yao, kuzorotesha maendeleo na kuchangia uhaba wa chakula.
Mashirika ya Umoja wa Mataifa yalionya wiki iliyopita kwamba zaidi ya nusu ya wakazi wa Sudan Kusini watakuwa na uhaba wa chakula katika msimu wa mwaka ujao unaoanza Aprili.