Idadi ya watu waliofariki katika tetemeko kubwa la ardhi nchini Myanmar na Thailand imepita watu Elfu Moja.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Dakika 1
Matangazo ya kibiashara
Watu wengine zaidi ya Elfu Mbili wameripotiwa kujeruhiwa katika tetemeko hilo la ardhi lenye ukubwa wa 7.7 ambalo liliripotiwa pia katika nchi jirani ya Thailand.
Hatua hii inakuja wakati huu ambapo idara za uokoaji zikiendelea kuwatafuta manusra katika vifusi vua majengo yalioporomoka.

Tetemeko hilo la ardhi liliharibu majengo, kuvunja madaraja pamoja na barabara nchini Myanmar.
Uharibifu mkubwa umeripotiwa katika Mji wa Mandalay, Mji wa pili kwa ukubwa nchini Mynmar unaokaliwa na watu zaidi ya Milioni 1.7.

Serikali ya kijeshi ya Myanmar ambayo imeekewa vikwazo na mataifa ya Magharibi imetoa ombi la msaada wa kimataifa.
Inaelezwa kwamba uongozi mkali wa jeshi la Myanmar na kuendelea kukosekana kwa utulivu wa ndani kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo kunafanya kuwa vigumu kupata taarifa sahihi kuhusu maafa hayo.

Hili ndilo lilikuwa tetemeko kubwa zaidi kuwahi kuripotiwa nchini Myanmar katika kipindi cha miongo kadhaa, kulingana na wanajiolojia, ambapo lilikuwa na uwezo wa kuharibu majengo jijini Bangkok, mamia ya kilomita kutoka eneo kulikoripotiwa tetemeko lenyewe.