Watu wakamatwa kwa kukiuka amri ya kutotoka nje Los Angeles

Polisi katika mji wa Los Angeles walianza kuwakamata watu waliokusanyika ili kuendeleza maandamano ya kupinga amri ya Rais Donald Trump ambayo wanasema ni ya ukandamizaji wa wahamiaji.

Meya wa Los Angeles, Karen Bass, alitoa amri hiyo ya kutotoka nje baada ya siku kadhaa za maandamano makubwa, kupinga uvamizi na kisha kuwakamata watu unaofanywa na maafisa wa mamlaka ya Uhamiaji na Utekelezaji wa Forodha wa Marekani (ICE) hatua iliyosababisha mapigano kati ya waandamanaji na maafisa hao wa serikali waliosema walikuwa wanatekeleza sheria.

Marekani 2025 | Maandamano katika jiji la Los Angeles
Meya wa jiji la Los Angeles, Karen BassPicha: Mario Tama/Getty Images

Maandamano hayo yaliyoanza siku tano zilizopita katika jiji hilo la Los Angeles maarufu LA, la pili kwa ukubwa nchini Marekani yalikumbwa na matukio ya uporaji na uharibifu na kuhayaribu maandamano yaliyokuwa ya amani.

Soma pia:  Trump apeleka askari Los Angeles huku maandamano yakiendelea

Rais wa Marekani Donald Trump amesema matukio hayo ndio yaliyomfanya achukue hatua ya kushangaza ya kupeleka wanajeshi, ingawa uamuzi wake huo imepingwa vikali na gavana wa jimbo hilo Gavin Newsom. Gavana huyo wa chama cha Democratic, amemlaumu Trump kwa kutumia nguvu zaidi ya inavyohitajika. “Trump anatumia nguvu za kijeshi kote Los Angeles, hatua hii inavuka mipaka ya dhamira yake ya kuwasaka wahalifu. Mawakala wake wanawakamata hadi waosha vyombo, watunza bustani, vibarua na hata washonaji. Huo ni udhaifu tu. Serikali ya Donald Trump hailindi jamii zetu badala yake jamii inatiwa inawatia kiwewe. Na hilo linaonekana kuwa ni lengo kuu.”

Rais Trump amewaamuru wanajeshi wapatao 4,000 kwenda Los Angeles, pamoja na Wanamaji 700 akidai kwamba amelazimika kuchukua hatua hiyo ili kudhibiti hali katika jiji hilo licha ya vikosi vya usalama vya jiji hilo kusema kuwa vyenyewe vinaweza kuidhibiti hali na kutuliza matukio yanayoendelea kwa sasa.

Washington 2025 | Rais wa Marekani Donald Trump
Rais wa Marekani Donald TrumpPicha: Ken Cedeno/Pool/Sipa USA/picture alliance

Soma pia: Trump atuma wanajeshi kuwadhibiti waandamanaji wahamiaji LA 

Rais wa Marekani Donald Trump ameapa ‘kulikomboa’ jiji la Los Angeles wakati ambapo maandamano yanaendelea kupinga operesheni za mamlaka ya Uhamiaji na Utekelezaji wa Forodha wa Marekani (ICE) dhidi ya wahamiaji walio nchini Marekani bila vibali.

Vyanzo: AFP/AP

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *