Watu milioni 7.3 waugua Malaria Ethiopia; 1,157 waaga dunia katika miezi 9

Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza kuwa, watu zaidi ya milioni 7.3 wamepatwa na ugonjwa wa Malaria nchini Ethiopia huku wagonjwa 1,157 wakiaga dunia kwa ugonjwa huo kuanzia Januari Mosi hadi Oktoba 20 mwaka huu.

Katika ripoti yake ya milipuko ya magonjwa, shirika la WHO limeeleza kuwa hii ni idadi kubwa zaidi ya wagonjwa wa Malaria kwa mwaka iliyosajiliwa katika kipindi cha miaka saba iliyopita.

Shirika la Afya Duniani limeongeza kuwa, ugonjwa wa Malaria pia unaweza kuambukizwa kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto kabla au wakati wa kujifungua na kwamba ni changamoto kubwa kwa afya ya umma nchini Ethiopia. 

Mbu jike aina ya Anopheles anayesababisha Malaria 

Ripoti ya WHO imeeleza kuwa majimbo  manne ya Ethiopia yamechangia  asilimia 81 ya wagonjwa wa Malaria walioripotiwa  na asilimia 89 ya  vifo vilivyosababishwa na ugonjwa huo katika mwaka huu wa 2024. Majimbo hayo ni  Oromia, Amhara, Jimbo la Kusini Magharibi na la Kusini mwa Ethiopia.

“Tunatoa msaada kwa Wizara ya Afya ya Ethiopia ili kuratibu juhudi za kukabiliana na Malaria kupitia majukwaa jumuishi na mfumo wa kushughulikia matukio mbalimbali ya dharura”, limesema Shirika la Afya Duniani.