Watu Milioni 4 waikimbia Sudan tangu kuanza kwa vita

Vita hivyo vinahusisha mapambano makali ya kuwania madaraka kati ya jeshi rasmi la Sudan na kikosi cha wanamgambo wa kikosi cha Rapid Support Forces, RSF. Maelfu wameuawa, na mamilioni wengine wameathirika kutokana na njaa na kukosa makaazi. Msemaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi (UNHCR) Eujin Byun, amesema Sudan imeingia mwaka wa tatu wa vita huku wakimbizi wakivuka milioni nne.

Kwa mujibu wa takwimu mpya, watu milioni 1.5 wamekimbilia Misri, zaidi ya milioni 1.1 wameingia Sudan Kusini—wakiwemo karibu wakimbizi 800,000 waliokuwa wanaishi Sudan—na wengine zaidi ya 850,000 wameingia Chad. Nchi jirani zimelemewa na idadi hii kubwa ya wahamiaji wanaoendelea kumiminika.

Mapigano makali yazuka kati ya jeshi la Sudan na RSF karibu na mji mkuu Khartoum

Nchini Chad, idadi ya wakimbizi kutoka Sudan imeongezeka mara tatu, kufikia zaidi ya milioni 1.2. Mratibu wa UNHCR nchini humo, Dossou Patrice Ahouansou, amesema hali hiyo imepita uwezo wa Chad kuhimili, huku makundi ya watu yakiendelea kuvuka mpaka kufuatia mashambulizi ya karibuni Kaskazini mwa Darfur.

Ahouansou amesema wakimbizi wengi wanafika wakiwa katika hali mbaya, wakikumbwa na ukosefu wa hifadhi, usalama mdogo, uhaba wa maji, na hali ya hewa kali. Amesema misaada ya dharura imekumbwa na upungufu mkubwa wa ufadhili, na kuitaka jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua dhidi ya ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu unaoendelea Sudan.

Vita vya wenyewe kwa wenyewe Sudan vimeigawa nchi kwa kiasi kukubwa

Sudan Khartoum | vita vya wenyewe kwa wenyewe Sudan
Mapigano makali yamekuwa yakiendelea sudan kati ya jeshi la serikali na wanamgambo wa RSFPicha: Osman Bakir/Anadolu/picture alliance

Vita hivyo vimeigawanya Sudan kimamlaka: jeshi linadhibiti mashariki, kaskazini na maeneo ya kati ya nchi, huku RSF na washirika wake wakitawala karibu maeneo yote ya Darfur na baadhi ya maeneo ya kusini. Mgawanyiko huu umeongeza ugumu wa kupeleka misaada ya kibinadamu.

Katika tukio la hivi karibuni, msafara wa misaada ya UN uliokuwa ukielekea mji wa El-Fasher mkoani Darfur Kaskazini ulivamiwa katika eneo la Al-Koma. Shirika la UNICEF limesema magari yao ya misaada yalishambuliwa, lakini halijaweka wazi ni nani aliyewashambulia. Pande zote mbili — jeshi na RSF — zimekanusha kuhusika na kushutumiana.

Mji wa El-Fasher, ambao ni mji pekee mkuu wa Darfur ambao haujatekewa na RSF, umekuwa chini ya mzingiro kwa zaidi ya mwaka mmoja. RSF imekuwa ikifanya mashambulizi ya mizinga kwenye mji huo na kambi za wakimbizi karibu nao, na kuua mamia ya raia huku ikitafuta kudhibiti Darfur yote baada ya kupoteza mji mkuu wa Khartoum mwezi Machi.

Wanamgambo wa RSF wazishambulia hospitali El-Obeid

Pande zote zinatuhumiwa kutumia njaa kama silaha ya kivita kwa kuzuia misaada na kuwashambulia raia. Umoja wa Mataifa unasema watu zaidi ya milioni 13 wamelazimika kuhama makazi yao. Katika jimbo la Darfur Kaskazini pekee, zaidi ya watu milioni moja wanakabiliwa na njaa kali.

Wakati vita vikiingia mwaka wa tatu, mashirika ya misaada yanasema kuwa bila ongezeko kubwa la fedha na shinikizo la kidiplomasia kufanikisha amani, hali ya kibinadamu itazidi kuwa mbaya. Kwa sasa, hali nchini Sudan inatajwa kuwa mojawapo ya janga kubwa zaidi la binadamu duniani.

reuters,ap,afp

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *