
Watu milioni 28 wanakabiliwa na njaa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, hii ikiwa idadi ya juu zaidi kwa nchi hiyo, inayochochewa na mzozo unaoendelea kati ya serikali na waasi wanaoungwa mkono na Rwanda mashariki mwa nchi hiyo, Umoja wa Mataifa umesema.
Imechapishwa:
Dakika 1
Matangazo ya kibiashara
UN inasema watu milioni 2.5 wanakabiliwa na njaa tangu kutokea kwa ghasia za mwezi Disemba na mwanzoni mwa mwaka huu, Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) na Shirika la Chakula na Kilimo (FAO) yamesema katika taarifa ya pamoja.
Mapigano kati ya vikosi vya serikali na waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda yameongezeka tangu mwanzoni mwa mwaka huu ambapo mamia kwa maelfu ya raia wamekimbia makazi yao.
Aidha katika taarifa yao mashirika haya yanasema zaidi ya watu milioni 10 ya wale wanaokabiliwa na njaa wako mashariki mwa Kongo, ambako kunashuhudia ukosefu wa usalama tangu vita vya baada ya mauaji ya kimbari ya 1994 yaliyosababisha vifo vya mamilioni ya watu na kusababisha kuundwa kwa mamia ya makundi ya wanamgambo mashariki mwa Congo.