Watu 50 wauawa katika shambulizi la kijeshi nchini Sudan

Zaidi ya watu 50 waliuawa na zaidi ya wengine 200 kujeruhiwa siku ya Ijumaa katika shambulio lililofanywa na Wanajeshi wa kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) kwenye kijiji kimoja katikati mwa Sudan.

Siku ya Ijumaa asubuhi, wanamgambo wa RSF walishambulia kwa makombora kijiji cha Alseriha katika eneo la Al Kamlin ambapo zaidi ya raia 53 wa kijiji hicho waliuawa na wengine zaidi ya 200 kujeruhiwa, baadhi yao wakiwa katika hali mahututi.

Tangu alfajiri ya Ijumaa, kikosi cha RSF kilivamia kijiji cha Alseriha, kaskazini mwa Jimbo la Gezira, na kuweka silaha zake na mizinga juu ya majengo na kuanza kuwafyatulia risasi raia wasio na silaha, lilisema Kongamano la Gezira, ambalo ni kundi lisilo la serikali.

katika taarifa yake siku ya Ijumaa, Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan ililaani “kampeni za kulipiza kisasi” za (RSF) dhidi ya vijiji na miji ya jimbo la Gezira, .

Wizara jiyo ilisema kuwa (RSF)  inaendesha kampeni katika misingi ya kikabila na kikanda, ambayo ni sawa na mauaji ya halaiki na mauaji ya kikabila.

Sudan imeharibiwa na mzozo mbaya kati ya Wanajeshi wa Sudan na RSF tangu katikati ya Aprili 2023. Mzozo huo umesababisha vifo vya zaidi ya watu 24,850.