Watu 45 wauawa kwa imani za kishirikina mkoani Geita

Geita. Watu 45 wameuawa mkoani Geita kwa imani za kishirikina kwa kipindi cha mwaka 2021-24 huku umaskini na ukosefu wa elimu vikitajwa kuwa chanzo cha mauaji hayo.

Takwimu hizo zimetolewa na Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Elisante Ulomi wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo viongozi wa dini, siasa, mashirika yasiyo ya kiserikali, wasanii na waandishi wa habari ikilenga kuelimisha juu ya umuhimu wa ulinzi shirikishi.

Amesema wakati Mkoa wa Geita ukiwa na vifo 45 vitokanavyo na imani za kishirikina, utafiti uliofanywa na kituo cha sheria na haki za binadamu unaonyesha vifo hivyo vimepungua nchini kutoka 307 mwaka 2017 hadi 115 mwaka 2021.

Ulomi amesema bado elimu inahitajika hasa kipindi hiki cha kuelekea kwenye uchaguzi mkuu ambacho Jeshi la Polisi halitamani kusikia mauaji ya kishirikina yakiripotiwa kwa sababu tu za uchaguzi.
“Nasema ni ukosefu wa elimu kwa sababu mtu anadanganywa kuwa muuwe mtoto au bibi mzee halafu anaambiwa hatagundulika kwa sababu akimaliza anaenda kuoshwa dawa kwa mganga, kwa hali ya kawaida haikuingii akilini lakini matukio haya yapo na tunakutana nayo,”amesema Ulomi.

Kamishna wa Polisi anayesimamia ushirikishwaji wa jamii katika masuala ya usalama, Faustine Shilogile amesema hali ya uhalifu hasa mauaji ya kukata mapanga na yale ya walinzi yamepungua kwa kiasi kikubwa na hiyo imewezekana kutokana na ushirikiano baina ya polisi na wananchi.

“Naomba muendelee kutoa ushirikiano huohuo wa karibu sehemu yoyote ikiwa na matukio ya uhalifu hapawezi kuwa na amani na shughuli za maendeleo haziwezi kufanyika, kila mmoja atakuwa anaogopa lakini kwa sasa Geita hali ni nzuri na machache yaliyobaki bado tunaweza kuyazuia,”amesema Shilogile.

Amesema Jeshi la Polisi limeamua kushirikisha jamii kubaini, kuzuia na kupambana na uhalifu kutokana na kubaini kuwa kupambana na uhalifu bila kushirikisha jamii uhalifu hautamalizika.

Akizungumza katika mafunzo hayo mwakilishi kutoka GGML, Mihinzo Tumbo ambaye ni mkuu wa kitengo cha polisi jamii amesema wameamua kushirikiana na Jeshi la Polisi kusaidia programu hiyo, ili kuhakikisha mkoa unakuwa salama.

Amesema katika kuimarisha ulinzi shirikishi vijana zaidi ya 900 kutoka vijiji 32 vinavyozunguka mgodi huo wameajiriwa kama polisi jamii na kupitia ajira hizo, vijiji vimenufaika kwa kuanzisha miradi ya maendeleo na vitega uchumi kwa ajili ya maendeleo ya wananchi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Safia Jongo amesema asilimia 80 ya mauaji yanayotokea mkoani Geita yanachangiwa na imani za kishirikina.

Safia amesema katika uchaguzi mkuu ujao jeshi hilo halitamani kutumia mabomu wala risasi, hivyo kupitia mafunzo hayo wataelimisha umuhimu wa amani na usalama.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *