
Takriban watu 45, wakiwemo watalii 31 na wafanyakazi 14 wametoweka baada ya boti yao kuzama katika eneo la kaskazini mwa mji wa Marsa Alam wa Bahari Nyekundu kwenye mkoa wa Bahari Nyekundu nchni Misri.
Amro Hanfy, gavana wa Jimbo la Bahari Nyekundu ametangaza habari hiyo iliyochapishwa jana kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook na kuongeza kwa kusema: “Baadhi ya manusura wamepatikana na kupelekwa kwa ndege kwa ajili ya matibabu. Juhudi kubwa zinaendelea za kuwatafuta waliopotea kwa msaada wa jeshi na wanamaji la Misri.”
Mkuu huyo wa mkoa wa Bahari Nyekundu amewataka watu walioko karibu na eneo la ajali kukaa mbali na eneo hilo ili kikosi cha uokoaji kiweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo.
Kwa mujibu wa taarifa za awali, boti hiyo ilizama karibu na mwamba wa matumbawe kaskazini mwa mji wa Marsa Alam.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, kituo cha kushughulikia majanga cha mkoa wa Bahari Nyekundu kilipokea ishara ya kuzuka hitilafu katika boti hiyo iitwayo Sea Story jana Jumatatu na kuanza kuchukua hatua za uokoaji.
Boti hiyo iliondoka Port Ghalib huko Marsa Alam juzi Jumapili Novemba 24 na ilitarajiwa kurejea Hurghada Marina tarehe 29 mwezi huu wa Novemba.