Takriban watu 30 wamefariki kutokana na mafuriko huko Kinshasa, mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, waziri wa afya wa mkoa huo ametangaza Jumapili, huku mvua kubwa iliyonyesha mwishoni mwa juma ikiharibu nyumba na barabara.
Imechapishwa:
Dakika 1
Matangazo ya kibiashara
“Idadi hii ni ya muda, lakini kwa sasa tunahesabu takriban vifo thelathini,” Patrician Gongo Abakazi ameliambia shirika la habari la REUTERS limesema.
Mto Ndjili, ambao unapitia sehemu ya jiji la takriban watu milioni 17, ulipasua kingo zake siku ya Ijumaa jioni, na kuziba barabara kuu ya taifa na kuwaacha waendeshaji magari wakiwa wamekwama tangu Jumamosi usiku.
“Jana usiku tukiwa tunarudi kutoka uwanja wa ndege kukutana na rafiki yetu, tulilala kwenye gari kwa sababu hapakuwa na sehemu salama ya kuegesha gari,” amesema mkazi wa Kinshasa, Patricia Mikonga.
Vitongoji kadhaa havikuwa na umeme.
Kerene Yala mkazi wa Makala wilayani humo amesema tatizo kubwa katika eneo hilo ni kukatika kwa maji.

Gavana wa mkoa wa Kinshasa Daniel Bumba Lubaki alisema miundo msingi ya maji imeathirika, lakini vifaa vitarejeshwa ndani ya siku mbili au tatu.
Katika hotuba yake kwenye televisheni, alilaumu vifo vingine kutokana na makazi haramu na kutishia kuwafurusha wakazi wa vitongoji visivyo na maendeleo.
Daktari Raphael Tshimanga Muamba ambaye ni mtaalamu wa masuala ya maji, amesema mto huo umeathiriwa na shughuli za binadamu kwa muda mrefu.
“Haya ni matendo ya binadamu ambayo yanaharibu mikondo ya maji; “Vipimo vyao havionyeshi tena uwezo wao wa awali wa kuzuia mafuriko,” ameliambia shirika la habari la REUTERS.
Mafuriko haya yanakuja wakati muhimu kwa nchi hii ya Afrika ya kati.Waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda wamezidisha mashambulizi yao mashariki mwa nchi tangu mwanzoni mwa mwaka, na kuua zaidi ya watu 7,000 katika miezi miwili ya kwanza ya mapigano katika mwaka huu.