Watoto 50 ni kati ya watu 84 waliouawa katika ‘mauaji ya halaiki ya kikatili’ iliyofanya Israel Ghaza

Wapalestina 84 wakiwemo watoto zaidi ya 50 wameuliwa shahidi katika mashambulizi mawili ya kinyama yaliyofanywa na jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya majengo ya makazi ya raia kaskazini mwa Ukanda wa Ghaza.

Ofisi ya Habari ya Serikali ya Palestina katika Ukanda wa Ghaza imeeleza katika taarifa kwamba, jeshi la Israel limefanya mauaji mawili ya kikatili kwa kuripua majengo ya makazi ya familia ya Shalayel na Ghandour kaskazini mwa ukanda huo na kuathiri zaidi ya raia 170, ambapo 84 kati yao wakiwemo zaidi ya watoto 50 wameuawa shahidi na makumi ya wengine wamejeruhiwa mbali na wasiojulikana waliko. 

Taarifa hiyo imefafanua kuwa, watu 84 “wameuawa kwa umati” kwa sababu hakuna wafanyakazi wa ulinzi wa raia, huduma za matibabu au huduma zingine za usaidizi zinazopatikana katika eneo hilo huku kukiweko na mzingiro wa Israel na mwendelezo wa mashambulio ya mabomu na makombora.

Damu za watoto wasio na hatia zinamwagwa kila leo na jeshi la Kizayuni Ghaza

Ofisi ya Habari ya Serikali ya Palestina katika Ukanda wa Ghaza imesema, jinai hizo zinafaywa wakati jeshi la utawala ghasibu wa Kizayuni linalenga familia za raia katika majengo ya makazi yanayokaliwa na raia na watu waliolazimika kuyahama makazi yao, waliofikwa na kila aina ya masaibu. 

Taarifa ya ofisi hiyo imeendelea kubainisha: “hii inaambatana na kutokuwepo kwa timu za ulinzi wa kiraia, huduma za matibabu, au timu za misaada, kwa sababu zimekuwa zikilengwa na kushindwa kufanya kazi kutokana na uvamizi wa Israel wa karibu mwezi mmoja. Uhalifu huu unaandamana pia na kusambaratika kwa mfumo wa afya kaskazini mwa Ghaza, huku hospitali zikiwa zimeharibiwa na kushindwa kutoa huduma”.

Wakati huohuo, serikali ya Palestina katika Ukanda wa Ghaza imetoa wito kwa jamii ya kimataifa kutekeleza wajibu wake wa kuwalinda raia, na kusisitiza kuwa Israel na washirika wake, ambao ni Marekani, Ufaransa, Uingereza na Ujerumani zinabeba dhima ya “mauaji ya kimbari” yanayoendelea kufanywa huko Ghaza.

Mauaji ya kimbari yaliyoanzishwa na utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukanda wa Ghaza tangu Oktoba 7, 2023, hadi sasa yameshaua shahidi Wapalestina 43,259 na kujeruhi 101,827…/