Watoto 36 wapoteza maisha kwa malaria Sudan Kusini katika muda wa wiki 2

Afisa wa ngazi ya juu wa serikali ya Sudan Kusini jana Jumanne alithibitisha kupoteza maisha watu 41 kutokana na ugonjwa wa malaria ,36 wakiwa ni watoto katika mji wa Pibor nchini humo.

Oleyo Akuer amesema kuwa watu 41 wamepoteza maisha na wengine 200 wamelazwa hospitali katika kaunti ya Likwangole katika muda wa wiki mbili zilizopita kufuatia kuenea ugonjwa wa malaria katika eneo hilo. 

Amesema, aghalabu ya wahanga wamepoteza maisha nje ya mji wa Likwangole na kwamba wagonjwa 200 wa malaria sasa wanapatiwa matibabu katika kituo cha afya huko Likwangole. Amesema kituo hicho hata hivyo kinasumbuliwa na uhaba wa dawa kutokana na tatizo la muda mrefu la ugavi.   

Malaria inaendelea kusababisha vifo nchini Sudan Kusini, hasa miongoni mwa watoto.

Wizara ya Afya ya nchi hiyo Julai mwaka huu ilizindua mpango wa chanjo ya malaria iliyolenga watoto wapatao 265,000 katika kaunti 28 katika majimbo sita ya Sudan Kusini.

Zoezi la utoaji chanjo ya malaria nchini Sudan Kusini 

Mwaka 2022, Sudan Kusini ilisajili wagonjwa wa malaria wasiopungua milioni mbili na laki nane na vifo 6,680 vilivyosababisha na ugonjwa huo.