Watia nia tisa waonywa CCM, yawashukia wanaogawa rushwa Kahama

Kahama. Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kahama, mkoani Shinyanga, kimeweka bayana msimamo wake  dhidi ya vitendo vya rushwa vinavyofanywa na baadhi ya watia nia wa nafasi za udiwani na ubunge katika kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.

Taarifa kutoka uongozi wa chama hicho zinaeleza kuwa jumla ya wagombea tisa tayari wamebainika wakijihusisha na vitendo vya kugawa fedha kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM nyakati za usiku, kinyume na maadili ya chama.

Katibu wa CCM Wilaya ya Kahama, Andrew Chatwanga, akizungumza na wanahabari leo Mei 9, 2025, amefichua kuwa wagombea hao wanatoka kwenye majimbo yote matatu ya wilaya hiyo: Kahama Mjini (watano), Ushetu (wawili) na Msalala (wawili).

Amesema vitendo hivyo si tu vinakiuka taratibu za chama, bali pia vinadhihirisha dharau kwa wajumbe na kudhalilisha dhamira ya chama ya kuwa na viongozi wanaokubalika na wananchi kwa uwezo na si kwa fedha.

“Tumebaini baadhi ya watia nia wanazunguka usiku kwa kata mbalimbali kuwapa wajumbe fedha, wengine hadi Sh10,000 ili wawapitishe kwenye mchakato wa ndani. Hii ni aibu, ni udhalilishaji na ni kinyume cha maadili ya CCM. Chama hakiwezi kumvumilia mgombea wa aina hiyo,” amesema Chatwanga.

Amesisitiza kuwa taarifa za wagombea waliobainika zimewasilishwa katika ngazi za juu za chama mkoani na makao makuu, na kuonya kuwa yeyote atakayebainika kuendelea na vitendo hivyo ataondolewa kwenye mchakato hata kabla ya kuchukua fomu.

Chatwanga amewaonya pia makatibu wa matawi wanaokumbatia wagombea na kudai kuwa ni “wagombea wao”, akisema chama hakiwezi kuvumilia viongozi wa aina hiyo wanaoeneza makundi na ushawishi wa kifisadi.

Kauli ya CCM Taifa

Akizungumza katika ziara zake kwenye mikoa ya Lindi, Mtwara, Morogoro na Dar es Salaam, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amosi Makalla amekemea vitendo vya rushwa ndani ya chama, akiwataka wanachama kuwa makini kuchagua viongozi kwa misingi ya uadilifu na sio fedha.

“Rushwa huharibu msingi wa demokrasia. Kama chama, hatutavumilia mgombea yeyote anayepenyeza fedha kama njia ya kupita. Tunahitaji viongozi wanaotumikia wananchi, si wanaotumia fedha kutafuta madaraka,” amesema Makalla.

Tahadhari kutoka Takukuru

Mapema Aprili 29, 2025, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Crispin Chalamila, alieleza kuwa taasisi hiyo imeanza kuchukua hatua kuhakikisha uchaguzi wa mwaka huu unakuwa huru na haki.

Alisisitiza kuwa rushwa si tu ni jinai, bali inavuruga misingi ya haki, usawa na uwajibikaji katika siasa.

“Tunahitaji wagombea wanaochaguliwa kwa uadilifu. Kupitia vyombo vya habari, tunataka jamii ielewe kuwa kutoa au kupokea rushwa ni kosa la jinai. Tutachukua hatua kali,” amesema Chalamila, akiongeza kuwa kuna mikakati kabambe inayotekelezwa kushughulikia mianya ya rushwa wakati huu wa kuelekea uchaguzi.

Maoni ya wananchi

Wakazi wa Kahama nao wameonyesha kuchoshwa na tabia ya wagombea kutumia fedha badala ya sera. Rose Chasama, mkazi wa Kahama Mjini, ameitaka Takukuru kuingilia kati haraka na kuchukua hatua dhidi ya wagombea wanaotoa rushwa.

“Wanaotoa fedha ndio wanaotuangusha baada ya kushinda. Hawarudi kwa wananchi na maendeleo yanazorota. Takukuru wasiwafumbie macho,” amesema.

Naye Rajabu Haruna wa Msalala amesema CCM inapaswa kuweka wazi majina ya wagombea waliobainika kutoa rushwa ili jamii iwaepuke hata wakati wa kupiga kura.

Mwongozo wa CCM

Kwa mujibu wa kanuni za CCM, mwanachama anayetaka kugombea nafasi yoyote ya uongozi anatakiwa kuchukua na kurejesha fomu katika eneo anakofahamika vizuri kitabia, kimahusiano, na kiutendaji kama mwanachama.

Vigezo vya uadilifu, uzalendo na utii kwa maadili ya chama ndio msingi mkuu wa kupitishwa kwake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *