Watendaji wachochezi waonywa Babati

Babati. Watendaji wa vijiji na Kata wa Wilaya ya Babati mkoani Manyara, wanaokiuka taratibu za kisheria katika masuala ya ardhi na kusababisha kuchochea migogoro ya ardhi isiyokuwa ya lazima wameonywa kuchukuliwa hatua kali.

Mkuu wa Wilaya ya Babati, Emmanuela Kaganda ametoa onyo hilo Aprili mosi mwaka 2025 kwenye Kata ya Ufana wakati akiwa kwenye ziara ya kutatua kero za wananchi hasa zinazohusu migogoro ya ardhi.

Kaganda amesema baadhi ya migogoro ya ardhi inachangiwa na watendaji wa Serikali wasiokuwa waaminifu ambao hushiriki katika uuzaji holela wa ardhi bila kufuata sheria.

Amesema Serikali haitawavumilia watendaji wa aina hiyo watakaobainika kufanya hivyo watachukuliwa hatua kali za kinidhamu na kisheria.

“Nataka kuwatahadharisha na kuwaonya watendaji wote wanaokiuka taratibu kwa kujihusisha na uchochezi na uuzaji holela wa ardhi kinyume na sheria,” amesema Kaganda.

Ameeleza kwamba vitendo vya uchochezi, rushwa, upendeleo na matumizi mabaya ya madaraka kamwe havitavumiliwa kwa mtumishi yeyote.

Ameeleza kwamba atachukua hatua kali kwa mtumishi yeyote atakayebainika kuhusika katika vitendo hivyo viovu visivyo na maadili.

Amewahimiza wananchi kuwa waaminifu na waadilifu katika maisha yao ya kila siku huku akionya tabia ya baadhi ya watu wanaowabambikizia kesi wenzao kwa maslahi binafsi.

Kaganda amesema tabia hiyo inasababisha uchochezi na migogoro isiyo ya lazima ndani ya jamii na kuchelewesha maendeleo.

“Migogoro mingi inayoripotiwa hapa inahusiana na ardhi na ni muhimu sana sisi sote kufuata sheria na taratibu zilizowekwa ili kuondoa matatizo haya,” ameonya.

Amekemea wanaotumia njia za udanganyifu kwa kuwasingizia wenzao makosa kwa manufaa yao binafsi, jambo ambalo halikubaliki na halitavumiliwa.

Mkazi wa Ufana, John Mayo amesema maagizo hayo ya mkuu huyo wa wilaya yakitekelezwa kama alivyoelekeza na yatafuatwa migogoro itapungua hasa ya ardhi.

“Hawa watumishi wa halmashauri hasa watendaji wa vijiji na kata wakiwa makini katika kufuatilia maagizo hayo migogoro itamalizika kama siyo kupungua,” amesema.

Mkazi mwingine Anna Paul amemshukuru mkuu huyo wa wilaya kufika kwenye kata hiyo na kutoa maelekezo ya Serikali ambayo anaamini yatawasaidia kuepuka unyanyasaji wa viongozi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *