Watatu wauawa Tabora kwa tuhuma za mauaji

Nzega. Watu watatu wameuawa na kisha kuchomwa moto na wananchi wenye hasira kali kwa tuhuma za kumuua kisha kumkata sehemu za siri pamoja na titi, Sagali Masanja (62), tukio lililotokea Novemba 14, 2024 katika Kijiji cha Mahene, Wilaya ya Nzega mkoani Tabora.

Waliouawa ni Masumbuko Ngassa (33), Shilinde Kaseko (30) pamoja na Sana Maganga (66) ambaye ni mama mzazi wa Shilinde.

Akizungumza na Mwananchi leo Novemba 14, 2024, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Richard Abwao amesema chanzo cha mauaji hayo ni imani za kishirikina.

Abwao amesema usiku wa kuamkia Novemba 14, 2024, mwanamke mmoja aliyefahamika kama Sagali Masanja (62) amefariki dunia baada ya kukatwa na panga sehemu mbalimbali za mwili wake kisha wauaji hao wakamkata titi moja la kushoto na sehemu za siri na kutokomea kusokojulikana.

Hata hivyo, Abwao amesema baada ya mauaji hayo kutokea, wananchi wa kijiji hicho walianza kuwafuatilia wauaji hao na kufanikiwa kuwakamata watu wawili waliofanya mauaji hayo wakiwa kwa mama mmoja mganga wa kienyeji aliyekuwa akiwazindika kwa kuwaosha dawa ili wasikamatwe katika Kijiji cha Seki, Wilaya ya Nzega mkoani hapa.

“Baada ya wananchi kufuatilia na kuwakamata, wale wauaji walikutwa na titi moja la binadamu, na sehemu za siri pamoja na vitu walivyoiba baada ya kufanya mauaji ikiwemo begi la nguo la marehemu ambapo wananchi wenye hasira kali walijichukulia sheria mkononi kwa kuwaua kisha kuwachoma moto wote watatu,” amesema Abwao.

Katika hatua nyingine, Abwao amesema baada ya Jeshi la Polisi kufika eneo la tukio baada ya kupata taarifa kutoka kwa wananchi, walifanikiwa kuwakamata watu watatu wakituhumiwa kuwatuma watuhumiwa wawili ambao ni Masumbuko Ngassa (33) pamoja na Shilinde Kaseko (30) kwenda kufanya mauaji hayo.

Waliokamatwa ni Lucia Mabula (36) ambaye ndiye aliyewatafuta wauaji na kuwalipa Sh200,000 na chanzo kikiwa ni imani za kishirikina kwamba mwanamke aliyeuawa katika Kijiji cha Mahene alikuwa mchawi na kwamba alimroga mtoto wa Lucia aliyefariki kwa kutumbukia ndani ya kisima mwaka 2023. Wa pili ni Makenzi Mabula ambaye ni mume wa Lucia (49) na watatu ni Ramadhan Kurwa (38).

“Watuhumiwa wote watatu wanashimiliwa na jeshi la Polisi kwaajili ya kuchukuliwa hatua kali za kisheria ikiwemo kuwafikisha mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili,” amesema Abwao.

Hata hivyo, Kamanda Abwao amesema jeshi hilo linatoa wito kwa wananchi wachache ambao bado wanaendekeza imani za kishirikina kuacha mara moja kwa kuwa zimekuwa zikisababisha madhara makubwa kwa binadamu.

“Tunatoa wito kwa wananchi wachache ambao wanaendekeza imani za kishirikina mkoani hapa  kuachanana na tabia hizo kwa sababu ni imani potofu zinazoongozwa na uongo mwingi lakini pia zinasabanisha madhara makubwa katika jamii, mfano zimesababisha mauaji ya watu wanne na wengine watatu kushikiliwa,” amesema Abwao.