Ushetu. Wachimbaji watatu wa dhahabu katika Kijiji cha Mwabomba, Wilaya ya Ushetu mkoani Shinyanga, wamefariki dunia baada ya kufukiwa na kifusi kwenye mgodi wa namba sita walilokuwa wakichimba.
Wanaotajwa kupoteza maisha katika tukio hilo ni Lotu Charles (31), Maneno Charles na Yakobo Tarima.
Kamanda wa Polisi mkoani Shinyanga Janeth Magomi amesema tukio hilo limetokea Aprili 17, 2025, saa 12 jioni, huku chanzo cha awali kikitajwa kuwa ni mvua zinazoendelea kunyesha.
Magomi ametoa wito kwa wachimbaji kuchukua tahadhari wanapokuwa katika shughuli zao za uchimbaji kipindi hiki cha mvua zinazoendelea kunyesha kwa kuwatumia maofisa madini na wataalamu waliopo kuwapa elimu ya uchimbaji unaozingatia usalama wao.
“Wachimbaji hawa walifunikwa na kifusi cha udongo wakati wakichimba dhahabu eneo namba sita na wamepoteza maisha. Tunaendelea kuchunguza lakini sasa hivi ni kipindi cha mvua, haraka haraka tu utaona kuwa udongo ulikuwa umelowana,”amesema Magomi.

Mwendesha pikipiki Yohana Maziku akiwa amebeba majeneza yatakayohifadhia miili ya wachimbaji watatu wa dhahabu waliofariki dunia baada ya kufukiwa na kifusi katika Kijiji cha Mwabomba Kata ya Idahina, Wilaya ya kipolisi Ushetu mkoani Shinyanga Aprili 17.
Diwani wa Idahina, Mathias Makashi amewasihi wamiliki wa maduara kuhakikisha usalama kabla ya kuwaruhusu vijana kuingia kuchimba ili kuzuia vifo vya mara kwa mara vinavyosababishwa na ubora mdogo wa maduara.
Ameishukuru Serikali kwa kuitambua sekta ya wachimbaji wadogo na kuendelea kuwapa leseni.
‘’Wito wangu ni kwamba wamiliki wa maduara waendelee kuimarisha hali ya usalama kwa wachimbaji wao, maduara yakaguliwe, yafungwe matimba yaliyo imara kila wakati, lakini pia hawa wachimbaji wapewe vitu vya kujikinga na ajali,” amesema.