Watatu wa familia moja wafariki dunia Chato

Geita. Watu watatu, akiwemo mtoto mdogo, wanaosadikiwa kuwa ni wa familia moja, wamepoteza maisha baada ya kugongwa na gari katika barabara ya Mganza – Chato, eneo la Nyabilele, Kata ya Mganza, wilayani Chato, Mkoa wa Geita.

Watu hao, waliokuwa wakitembea kwa miguu, ni mwanaume pamoja na mwanamke aliyekuwa amebeba mtoto mgongoni.

Hata hivyo, majina yao bado hayajatambuliwa, ingawa inadaiwa kuwa ni wa familia moja waliohamia katika eneo hilo siku za karibuni.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Safia Jongo, amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema kuwa ilitokea Aprili 2, 2025.

Miili ya marehemu imehifadhiwa katika Kituo cha Afya Mugaza, Chato, kwa taratibu za uchunguzi na utambuzi.

Akielezea tukio hilo, Kamanda Jongo amesema dereva aliyeendesha gari hilo alikimbia baada ya kusababisha ajali na Jeshi la Polisi linaendelea kumsaka.

Aidha, Jongo amemtaka dereva na mmiliki wa gari hilo kujisalimisha katika kituo chochote cha polisi kwa ajili ya hatua za kisheria.

Pia,  amewataka wananchi kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi endapo watabaini uwepo wa gari iliyopata ajali katika maeneo yao.

Wakati huohuo, Jeshi la Polisi linamshikilia Abel Josephat (43), mkazi wa Nyamirembe, wilayani Chato, kwa tuhuma za kupiga picha miili ya watu waliofariki dunia katika ajali hiyo na kuzisambaza kwenye mtandao wa kijamii (Instagram).

Kamanda Jongo amesema mtu huyo alisambaza maudhui yasiyokubalika, kitendo ambacho ni kinyume cha sheria.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *