Watatu mbaroni wakidaiwa kumuua dereva bodaboda Arusha

Arusha. Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha linawashikilia watu watatu kwa tuhuma za mauaji ya dereva bodadoda, Meijo Lemokolo (23), mkazi wa Kijiji cha Orbomba, Wilaya ya Longido mkoani Arusha.

Watuhumiwa waliokamatwa ni Omary Jumanne (31) ambaye ni mfugaji, Mohamed Ally (25) na Chricensia Haule (25) ambao ni wakulima wakazi wa Kijiji cha Shimbi wilayani Rombo Mkoa wa Kilimanjaro.

Akizungumzia tukio hilo leo, Jumanne Septemba 24, 2024, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo amesema watuhumiwa hao wanashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha kwa tuhuma za kutekeleza tukio hilo la mauaji Juni 21, 2024 Wilaya ya Longido.

“Tukio limetokea Juni 21, 2024 watuhumiwa hawa baada ya kumuua Meijo, walifanikiwa kuiba pikipiki aina ya Kinglion, mali ya marehemu,” amedai Kamanda Masejo.

Amedai kuwa, watuhumiwa walipotekeleza tukio hilo walikimbia na jeshi hilo lilianza upelelezi wake hadi Septemba walipofanikiwa kuwakamata watuhumiwa wote kwa nyakati tofauti huko Kilimanjaro katika Wilaya ya Rombo.

Kamanda Masejo amesema pikipiki ya marehemu imepatikana na imehifadhiwa kituoni kama kidhibiti katika taratibu za kisheria.

Amewataka wananchi kutoa taarifa viashiria au matukio pindi yanapotokea ili kutokomeza matukio ya uhalifu katika maeneo yao.