Watanzania wakiri ugumu wa Ligi Uturuki

WATANZANIA wawili wanaokipiga katika Ligi ya Walemavu nchini Uturuki wamesema msimu huu umekuwa mgumu kwenye timu zao.

Wachezaji hao ni Hebron Shadrack wa Sisli Yeditepe na Ramadhan Chomelo anayekipiga Konya Amputee wakiitumikia ligi hiyo kwa msimu wa tatu sasa.

Akizungumza na Mwanaspoti, Chomelo alisema ligi nchini humo imekuwa ngumu kutokana na ushindani unaoonyeshwa na baadhi ya timu.

“Nadhani ligi imeanza kuchangamka, msimu huu hatujaanza vizuri mechi nane, tumetoa sare moja na kupoteza mbili tukishinda tano tuna michezo mingine ya kurekebisha kwa kuwa mzunguko wa pili bado,” alisema.

Kwa upande wa Shadrack alisema anapokuwa nje timu inakumbana na changamoto nyingi kwenye eneo la kushambulia hivyo anapambana kuhakikisha hapati majeraha.

“Timu haiko sawa naweza kusema mimi ni kama tegemeo kwenye kikosi chetu ninapopata jeraha inakuwa changamoto na msimu huu nimebadilishwa nafasi kutoka kiungo hadi winga hadi sasa nina asisti sita na mabao matatu kwenye mechi nane.”