Watanzania wafundishwe sayansi ya data, AI kwa malengo

Watanzania wafundishwe sayansi ya data, AI kwa malengo

Data ni mafuta mapya.’ Ni msemo maarufu uliotolewa na mwanahisabati Clive Humby mwaka 2006. Kama yalivyo mafuta ya petroli, yamekuwa rasilimali yenye thamani kubwa, ndivyo data imegeuka kuwa kichocheo muhimu cha maendeleo ya uchumi wa kidijitali. Ulimwenguni kote, taasisi zinawekeza kwenye uchakataji wa data na matumizi ya akili bandia (AI).

Sayansi ya data na akili bandia si tu mada za kisayansi, bali ni nguvu mpya ya kiuchumi. Ndiyo maana mashirika ya umma na binafsi yanahangaika kuwapata wataalamu wa maeneo haya. Vyuo vikuu navyo vinapanua kozi zao ili kutoa elimu katika fani hizi. Akili bandia ni pana zaidi ya uelimishaji wa mashine (machine learning) kwa kuwa inajumuisha uwezo wa mashine kujifunza, kufikiri, na hata kuunda suluhisho kama binadamu.

Chuo Kikuu cha Howard, nilipoajiriwa, kimeanzisha kozi ya mtandaoni ya sayansi ya data inayopatikana kwa watu duniani kote. Hii ni miongoni mwa jitihada za vyuo mahiri duniani kuhakikisha elimu ya kisasa inawafikia wengi. Tanzania pia haipo nyuma. Chuo Kikuu cha Dar es Salaam sasa kinatoa Shahada ya Umahiri na Uzamivu katika Sayansi ya Data. Wahitimu wake wanatarajiwa kuwa viongozi wa mifumo ya data, wabunifu wa teknolojia, na wahadhiri.

Hata hivyo, kama Taifa bado tupo nyuma. Tuna upungufu wa wataalamu wengi wa fani hizi. Ingawa taasisi kama Jumuiya ya Akili Bandia Tanzania na Maabara ya Data Tanzania zinajitahidi, bado hatujafikia kasi ya nchi kama India, China, Rwanda, na hata Kenya.

Sababu mojawapo ni uhaba wa nafasi za masomo na changamoto ya ada. Lakini pia, hata zile nafasi zinazotolewa mahususi kwa Watanzania nje ya nchi haziwezi kutumika kikamilifu. Kwa mfano, katika nafasi 10 za Jumuiya ya Madola, ni Watanzania watatu hadi watano pekee wanaofanikiwa. Wengine hukosa kwa sababu maombi yao hayajaandikwa kwa ubora unaotakiwa.

Vivyo hivyo kwa China, ambayo hutoa hadi nafasi 120 kwa mwaka. Lakini Watanzania wanaofanikiwa ni wachache. Wengine hushindwa kumaliza kwa wakati, jambo linalosababisha nafasi kupunguzwa.

Urusi hutoa nafasi 90 na zote zinatumika, shukrani kwa uhamasishaji mzuri wa jumuiya ya wahitimu.

Mfano mzuri wa mafanikio ni asasi ya TanSAF (zamani TanSAO), iliyoanzishwa kusaidia wanafunzi waliopata alama za juu kuandika maombi bora ya udhamini.

Kwa juhudi hizo, vyuo vya hadhi kubwa kama Harvard na Princeton sasa vinadahili Watanzania zaidi kila mwaka. Kuna mfano wa mama mmoja aliyekuwa na furaha baada ya mwanawe, Arden Masige, kupata udahili katika vyuo vitano vikuu vya Marekani, mojawapo ikiwa Yale.

Nafasi zipo. Uwezo pia upo. Tunachokosa ni mifumo madhubuti ya kuwajengea uwezo vijana wetu kuzitumia fursa hizo. Waziri wa Elimu, Profesa Adolf Mkenda, katika hotuba ya bajeti ya 2025/2026, alitangaza mpango mpya wa Serikali wa kufadhili wanafunzi bora wa Kidato cha Sita kusomea Sayansi ya Data, Akili Bandia, na Uelimishaji wa Mashine nje ya nchi.

Watakaochaguliwa watawekwa kambini ili kuandaliwa kitaaluma kabla ya kutuma maombi ya udahili vyuoni. Mafunzo haya yatatolewa na wataalamu kutoka sekta za umma, binafsi, na Diaspora.

Kwa wale waliokwisha pata shahada ya kwanza, watapewa ufadhili kusomea shahada ya umahiri katika NM-AIST na IIT Madras Zanzibar, pamoja na kusaidiwa kuomba nafasi kwenye nchi kama Uingereza na China.

Mpango huu umepewa jina la Mama Samia 360 – DSP/AI+ ikiwa ni mwendelezo wa Mama Samia Extended Scholarship kwa masomo ya sayansi. Lengo ni kuwa na idadi kubwa ya wataalamu wa ndani wenye uwezo wa kimataifa katika nyanja za teknolojia ya kisasa.

Wakati wa kongamano la 18 la e-Learning Africa jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Udahili wa CMU-Afrika alieleza kushangazwa na idadi ndogo ya Watanzania wanaosoma kwenye tawi lao lililopo Rwanda. Jibu la haraka ni kwamba tunapenda lakini hatujawezeshwa vya kutosha.

Ni wazi kuwa tusipofanya juhudi za makusudi kuwekeza katika kizazi kipya cha wataalamu wa sayansi ya data na akili bandia, tutasalia kuwa watazamaji wa maendeleo ya kidijitali badala ya washiriki.

Ni lazima tufanye kila jitihada kuwaandaa vijana wetu, kwa sababu teknolojia hizi si za kesho tena, bali ni za leo.

Ili iweje? Ili tuwe na kizazi cha Kitanzania chenye uwezo wa kutumia teknolojia hizi kwa tija—na kwa haki.

Chambi Chachage ni Profesa Msaidizi katika Chuo Kikuu cha Howard, mtaalamu wa data na akili bandia, na mdau katika maendeleo ya elimu na ubunifu nchini Tanzania

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *